Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 17 Mei 2014 amewapongeza wanachama wa Chama
cha Wahudumu wa Msalaba, kinachoadhimisha Jubilee ya miaka mia moja tangu alipozaliwa
Mwenyeheri Padre Luigi Novarese, muasisi wa chama hiki.
Huyu ni Padre aliyeonesha
upendo wa dhati kwa Kristo na Kanisa lake, akajisadaka kwa ajili ya huduma makini
kwa wagonjwa. Ni Padre aliyeonja mateso na mahangaiko makubwa katika utoto wake, akajifunza
na kuguswa na mahangaiko ya binadamu, ndiyo maana akaanzisha Chama cha Wahudumu wa
Msalaba wanaotekeleza dhamana na utume wao katika hali ya ukimya pasi na makeke!
Wanachama
hawa walipokutana na Baba Mtakatifu walikuwa wameandamana na wagonjwa wanaowahudumia
wakiwa kwenye baiskeli maalum. Hawa Baba Mtakatifu amewashirikisha kwa namna ya pekee
heri za mlimani, muhtasari wa mafundisho ya Yesu, akisema heri wanaohuzunika sasa
maana hao watafarijiwa. Hawa ni watu ambao wanakabiliwa na matatizo ya afya, upweke,
kutoeleweka na kwamba, kuna sababu nyingi ambazo zinaweza kumpelekea mtu kushikwa
na majonzi na simanzi.
Hata hivyo wanapaswa kukumbuka kwamba, Yesu aliteseka
na kudharauliwa sana, akajitwika mabegani mwake mateso na mahangaiko ya binadamu hadi
mauti ya Msalaba. Yesu katika maisha yake hapa duniani ameonja mateso mengi, kiroho
na kimwili; ameonja uchovu na njaa; hali ya kutoeleweka, akasalitiwa na kukimbiwa
na Mitume wake, akachapwa mijeledi na hatimaye, akatundikwa na kufa Msalabani.
Baba
Mtakatifu anasema, mateso na mahangaiko ya watu si jambo la kufurahia lakini ni ukweli
ambao unamfunda mwanadamu kuishi kwa kuwa na mwelekeo sahihi wa maisha. Kuna baadhi
ya watu wanaoona mateso katika mwelekeo hasi kabisa, kiasi cha kujikatia tamaa na
kuasi, hali ambayo si nzuri hata kidogo anasema Baba Mtakatifu. Ukweli wa maisha,
mateso na mahangaiko ya binadamu hayana budi kupokelewa kwa imani na matumaini na
kuyarutubisha kwa upendo wa Mungu na jirani kwani upendo una nguvu ya kuleta mabadiliko
ya kweli!
Haya ndiyo mafundisho ya kina yaliyotolewa na Mwenyeheri Luigi Novarese
kwa kuwafundisha wagonjwa na walemavu kupokea na kuthamini mateso na mahangaiko yao
mintarafu mwelekeo wa kitume, unaowawezesha kutekeleza yote katika imani na mapendo
kwa jirani. Wagonjwa hawana budi kuwa ni wadau katika maisha na utume wao, kwani mgonjwa
au mlemavu anaweza kuwa ni mwanga angavu kwa watu wengine wanaoteseka, kiasi cha kuleta
mabadiliko makubwa katika mazingira ambamo wanaishi.
Baba Mtakatifu anawahakikishia
kwamba, kwa karama hii, wao kweli ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa. Mateso na mahangaiko
yao ni kama Madonda Matakatifu ya Yesu, ambayo kwa upande mmoja yanaonekana kuwa ni
kashfa katika imani lakini pia yanaimarisha imani, kielelezo kwamba, kweli Mungu ni
upendo, mwaminifu, mwenyehuruma na mfariji. Kwa kuungana na Yesu Kristo Mfufuka, wagonjwa
na walemavu hawa ni sehemu ya wokovu na mchakato wa Uinjilishaji.
Baba Mtakatifu
anawaalika na kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa karibu na
wote wanaoteseka kutokana na magonjwa, ili kuwaonjesha ushuhuda wa Kristo Mfufuka.
Kwa njia hii wataweza kulitajirisha Kanisa pamoja na kuendelea kushirikiana na wachungaji
wa Kanisa, kwa kusali na kutolea mateso na mahangaiko yao kwa ajili ya Kanisa.
Baba
Mtakatifu mwishoni, anawaombea ili Bikira Maria awasaidie kuwa kweli ni wafanyakazi
wa Fumbo la Msalaba na wahudumu wa mateso na mahangaiko ya binadamu kwa kujikita katika
imani na matumaini pamoja na kuendelea kushikamana na Kristo.