2014-05-16 11:45:34

Njia za kumfahamu Yesu: Sala, Sakramenti, Maisha adili na Matendo ya huruma!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa, tarehe16 Mei 2014 anasema kwamba, ili kumfahamu Yesu, kuna haja ya kusali kwa bidii kutoka katika undani wa moyo wa mwamini; kumwadhimisha kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na kumuiga kwa njia ya matendo adili na kwamba, waamini wanaweza kumfahamu vyema zaidi Yesu, ikiwa kama watajijengea utamaduni wa kusoma Maandiko Matakatifu.

Yesu mwenyewe amatangaza kwamba, ni njia, ukweli na uzima! Baba Mtakatifu anasema haitoshi kumjifunza Yesu darasani au kwa kusoma Katekesimu ya Kanisa Katoliki, bali kuhakikisha kwamba, wanamfahamu Yesu kwa kina na mapana, kwani kwa njia ya mawazo peke yake wanaweza kutumbukia katika uzuo hali ambayo inagumisha mchakato wa kumfahamu Yesu kwa dhati!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujifunza na kusali ili kuweza kumkaribia Yesu zaidi. Mabingwa wa taalimungu ni wale ambao wameandika kazi zao kwa kupiga magoti yaani kwa njia ya sala! Waamini wajifunze pia kushiriki katika maadhimisho ya Sakramenti na Ibada mbali mbali za Kanisa, kwani hapa wanachota nguvu na maisha mapya!

Yesu anawaimarisha katika Agano na kuwatuma kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Kwa njia hii, kweli waamini wanaweza kumfahamu Yesu Kristo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Injili ni muhtasari wa maisha na utume wa Yesu, mwaliko wa kulisoma, kulitafakari Neno la Mungu na kulimwlisha katika matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji. Kwa njia hii, waamini wanaweza kulitambua Fumbo la maisha ya Yesu, bila ya kuwa na woga wala mashaka. Ili kufanikisha azma hii kuna haja ya: kusali, kuadhimisha, kuishi na kumwilisha maisha ya Yesu katika matendo ili kukutana na ukweli na hatimaye kupata utimilifu wa maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.