2014-05-16 10:19:36

Ndoa si mkataba wa mpito!


Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia anasema, maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Mei ni fursa muhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia, kwa kuibua sera na mikakati itakayolinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Wanadiplomasia wanaoiwakilisha Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wanapenda kutoa mchango wao katika kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya familia, kwa kutambua na kuthamini familia kama chanzo cha maisha ya kijamii, rasilimali kuu katika maendeleo ya watu mintarafu kipimo cha ubinadamu.

Waamini walei, asema Askofu mkuu Paglia wanalojukumu la kuhakikisha kwamba, familia zao zinakuwa ni mfano bora wa kuigwa, kwa kutambua kwamba, upendo wao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa, kwa kujikita katika mshikamano wa dhati, ili kuonesha ile furaha ya maisha ya ndoa inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Familia za Kikristo zinaalikwa kwa namna ya pekee, kujibidisha kutoa malezi makini kwa watoto wao pamoja na kumwilisha imani katika matendo kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kimsingi anasema Askofu mkuu Paglia kwamba, familia za Kikristo zinatumwa kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani.

Kuna haja ya kujenga na kudumisha mahusiano ya dhati kati ya kizazi kimoja na kizazi kingine kwa njia ya mchakato wa elimu na malezi bora. Baba wa familia wanapaswa kutekeleza dhamana yao katika malezi, lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kutokana na sababu mbali mbali baadhi ya wanaume wanashindwa kutekeleza utume wao barabara hali ambayo inaweza kusababisha malezi tenge kwa watoto.

Familia zinapaswa kujikita katika umoja na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia nzima na kwamba, ndoa si mkataba wa mpito, bali ni hija ya maisha, hadi pale kifo kitakapowatenganisha kadiri ya mapenzi ya Mungu. Familia zijitahidi kufisha ubinafsi ili kujisadaka kwa ajili ya maendeleo yao na jamii inayowazunguka!







All the contents on this site are copyrighted ©.