Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anasema kwamba, hija ya kitume ya
Baba Mtakatifu Francisko nchini Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014
imesheheni utajiri mkubwa wa maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa majadiliano
ya kiekumene yaliyoanzishwa na Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI kwa kukutana, kuzungumza
na kusali na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu, miaka hamsini iliyopita.
Kilele
cha hija hii ya kiekumene ni pale Baba Mtakatifu Francisko watakapokutana na kusalimiana,
kuzungumza na kusali pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza, Jumapili jioni, kwenye
Kaburi Takatifu. Kuna matukio mengine muhimu sana katika hija hii ya kiekumene, adhimisho
la Ibada ya Misa Takatifu mjini Amman na ile itakayoadhimishwa kwenye Pango la Mtoto
Yesu mjini Bethlehemu pamoja na kutembelea maeneo makuu ya historia na maisha ya Yesu
hapa duniani.
Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu atakutakana na waamini,
viongozi wa Kanisa na Serikali pamoja na wawakilishi wa wahamiaji na wakimbizi walioko
huko Mashariki ya Kati, wanaohudumia kwenye kambi mbali mbali. Baba Mtakatifu akiwa
katika Nchi Takatifu atakutana na kuzungumza na Rabbi Abraham Skorka Rabbi mkuu kutoka
Argentina ambaye ataambatana na Bwana Omar Abboud, Rais waTaasisi ya Majadiliano ya
Kidini mjini Buenos Aires.