Nigeria yashutumiwa kwa kutaka kujadiliana na magaidi!
Serikali ya Nigeria imeonesha nia ya kutaka kujadiliana na Kikundi cha Kigaidi cha
Boko Haram, ili kupata muafaka utakaokiwezesha kikundi cha Boko Haram kuwaachilia
huru wasichana wa shule waliotekwa nyara, Kaskazini mwa Nigeria, jambo ambalo limeshutumiwa
vikali na Serikali ya Marekani kwa kusema kwamba, hakuna haja ya kuzungumza na magaidi!
Kwa
kipindi cha miaka minne, Boko Haram imehusika na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa
na hatia nchini Nigeria pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na
mali za watu. Serikali ya Nigeria ilianzisha opresheni maalum ya kuwasaka wanajeshi
wa Kikundi cha Boko Haram, lakini hadi sasa hakuna mafanikio yoyote na watu wanaendelea
kupoteza maisha yao.
Hivi karibuni, Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria aliomba
msaada kutoka kwenye Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, tayari kuna baadhi ya nchi zimekwishatuma
makachero wake kufanya kazi hii, ili kupambana na Kikundi cha Boko Haram. Hali ya
hatari iliyotangazwa na Serikali ya Nigeria kwa kipindi cha miezi sita, inafikia ukomo
wake, tarehe 15 Mei 2014! Kifuatacho nchini Nigeria bado kimebaki kuwa ni kitendawili!