Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini, limehitimisha Kongamano la Familia Kimataifa
Barani Asia, lililomshirikisha pia Askofu mkuu Jean Laffite, Katibu mkuu wa Baraza
la Kipapa la Familia aliyekazia umuhimu wa Jamii kulinda na kudumisha haki msingi
za maisha ya ndoa na familia kwa kujikita katika kuenzi uhai, tunu ambayo leo hii
iko hatarini kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na ubinafsi wa
baadhi ya watu ambao hawataki tena kuwajibika katika masuala ya ndoa na familia!
Askofu
mkuu Laffite anasema, mchako wa maandalizi na hatimaye wa maadhimisho ya Sinodi maalum
ya Maaskofu kwa ajili ya familia itakayofanyika katika awamu mbili kama alivyopanga
Baba Mtakatifu Francisko, ni kuliwezesha Kanisa kuangalia changamoto zinazoigusa familia
katika ulimwengu mamboleo. Ni fursa ya kuangalia ni jinsi gani Kanisa linaweza kuwasadia
wanandoa watarajiwa kujiandaa kikamilifu katika utekelezaji wa dhana na utume wao
katika ndoa na familia, kwa kukuza na kuimarisha utume wa familia.
Kongamano
hili limeongozwa na kauli mbiu "Familia Barani Asia, mwanga wa matumaini", jambo linaloonesha
matumaini ya Kanisa kwa ajili ya familia kwa siku za usoni, kwa kushiriki katika mchakato
wa Uinjilishaji mpya, kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea
Ufilippini.
Ni mwaliko wa kuinjilisha kwa kuonesha mshikamano wa familia zilizoungana,
familia zinazosimikwa katika imani, matumaini na mapendo, wakati wote wa maisha, kwa
kujikita katika Sakramenti za Kanisa pamoja na kuendelea kujitajirisha kwa tafakari
ya Neno la Mungu, linalomwilishwa katika matendo ya huruma! Familia za Kikristo zioneshe
ile furaha na matumaini yanayobubujika kutoka katika maisha ya ndoa na familia, kwa
kukazia pia maisha ya pamoja, mahali ambapo watu wanashirikishana mang'amuzi na kweli
za maisha.
Askofu mkuu Laffite katika hotuba yake amegusia kwa kina na mapana
kuhusu "Mwongozo wa Haki Msingi za Kifamilia", Waraka ambao ulikuwa umeandaliwa na
Mtakatifu Yohane Paulo II kwa ajili ya Familia, lakini hakufanikiwa kuuchapa hadharani
kama mwongozo wa Kanisa kuhusiana na utume wa familia ndani ya Kanisa na Jamii katika
ujumla wake. Ameangalia umuhimu wa familia na ndoa kama taasisi kadiri ya sheria.
Mtakatifu Yohane Paulo II alipenda kukazia kwa namna ya pekee haki msingi
za kifamilia zinazofumbatwa katika asili ya familia. Hizi ni haki zinazopaswa kuheshimiwa,
kulindwa na kuendelezwa. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kukuza na kuendeleza sera
makini kwa ajili ya ndoa na familia.