2014-05-15 07:02:07

Familia ni shule ya kwanza ya tunu msingi za kiutu


Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia yuko kwenye ziara ya kikazi mjini Philadelphia, Marekani ili kuangalia maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa, yatakaofanyika mjini Philadelphia, kunako mwaka 2015. Akiwa nchini Marekani, Alhamis, tarehe 15 Mei, 2014 anashiriki katika maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa, miaka ishirini iliyopita. RealAudioMP3

Askofu mkuu Paglia anasema, maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa kwa ajili ya Kanisa yanakwenda sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya maalum ya Maaskofu Katoliki, iliyoitishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2014 na Mwaka 2015, ili kuweza kuyaangalia matatizo, changamoto, fursa na hatimaye, Kanisa kwa ujumla baada ya tafakari ya kina, liweze kuibua mbinu mkakati kwa ajili ya maisha na utume wa Familia ndani na nje ya Kanisa.

Familia zimepewa msukumo wa pekee kufanya tafakari ya kina kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo ndani na nje ya Kanisa, lakini zaidi katika ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknlojia. Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, maadhimisho ya Sinodi hizi, utakuwa ni mwanzo mpya kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, kuna haja kwa familia, parokia na vyama vya kitume kushiriki kikamilifu katika kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa njia ya ushuhuda makini na wenye mvuto na mashiko, changamoto kwa tamaduni na dhana ambazo kwa sasa zinaonekana kuwa ni tishio kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Askofu mkuu Paglia anasema, ni wajibu wa Familia za Kikristo kuandika barua ya furaha inayoandikwa si kwenye karatasi, bali kutoka katika undani wa maisha ya wanafamilia wenyewe katika maeneo yao! Hii ni barua inayopaswa kusomwa na wengi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Hapa Familia zinaalikwa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na hali ya kukata tamaa.

Wanafamilia wanaalikwa kujiondoa kutoka kwenye ubinafsi, kwa kushiriki katika kazi ya uumbaji, malezi na matunzo kwa watoto wao. Waamini katika ujumla wao wasaidie ujenzi na uimarishaji wa tunu bora za maisha ya ndoa na familia. Wawarithishe vijana wa kizazi kipya umuhimu wa kuthamini na kuendeleza maisha ya ndoa na familia pamoja na kuendelea kujikita katika: upendo, mshikamano; tunu msingi za maisha ya Kijamii na Kikanisa.
Wazee wapewe heshima katika Jamii kwa kutambua kwamba, vijana kwa sasa wanachezea maisha, lakini fainali ni uzeeni. Wazee washirikishwe katika maisha na tamaduni za watu, kwa kupewa huduma bora za tiba. Kuna haja ya kuwa na uhusiano mzuri kati ya kazi na familia; kwa kuimarisha maisha ya kiroho kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti na Matendo ya huruma.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia anasema kwamba, inasikitisha kuona kuwa baadhi ya watu wana dhana potofu kuhusu maisha ya ndoa na familia. Wanadhani kwamba, ndoa ni mkataba wa mufa mfupi; ndoa ni ndoana ya kutafuta umaarufu, utajiri na mali, ndoa si tena muungano thabiti kati ya Bwana na Bibi katika maisha yote, kwa kusaidiana wakati wa raha na shida, hadi kifo kitakapowatenganisha.

Jamii inawajibika kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa familia bora, shule ya kwanza ya tunu msingi za kiutu, kiroho na kitamaduni. Pale ambapo familia inawekwa rehani, hapo maisha ya wengi yako mashakani!








All the contents on this site are copyrighted ©.