Mahakama moja nchini Sudan imemkuta na hatia Meriam Yahya Ibrahim Ishaq, mwanamke
mwenye umri wa miaka 27 ya kukufuru na kuzini kwa kuwa ameolewa na raia mmoja Mkristo
kutoka Sudan ya Kusini na hivyo kuhukumiwa kuchapwa viboko mia moja na kunyongwa hadi
kufa!
Adhabu hii imewashtua watetezi wa haki msingi za binadamu, kwa kuitaka
Serikali ya Sudan kuheshimu uhuru wa kuabudu kadiri ya Katiba ya nchi iliyotungwa
kunako Mwaka 2005.
Mahakama hiyo imetumia "Sharia" za dini ya Kiislam zilizoingizwa
nchini humo kunako mwaka 1983 zinazopiga rufuku kwa mwamini wa dini ya Kiislam kuoa
au kuolewa na Mkristo. Viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wameitaka Serikali
ya Sudan kuingilia kati ili kusitisha utekelezaji wa adhabu hii ambayo ni kinyume
cha haki msingi za binadamu.