2014-05-14 06:50:05

Nyumba ya Mkate!


Jina hili Bethlehemu linatokana na maneno mawili ya Kiebrania, Bet ni nyumba na Lehem (lexem) ni mkate, kwa hiyo Beth-Lehem au bet-lexem maana yake nyumba ya mkate. RealAudioMP3

Kwa lugha ya kigiriki cha zamani walitamka Bethleem. Ziko sehemu nyingi zenye nyumba ya mkate mathalani Beth-lehem-ephratah, Bethlehemjudah, lakini Bethlehemu iliyokuwa kusini karibu na Yerusalemu ndiyo iliyokuwa inaitwa Bethlehemu katika mji wa Daudi. Hapo ndipo alipozaliwa Yesu. Ni mji ambao toka zamani wameishi wakristu wengi, lakini sasa wanaishi pia watu wa dini mchanganyiko. Sehemu hii wanafurika wahaji na watalii wengi sana hususani wakati wa Kipindi cha Noeli.

Kisa cha kujulikana Betlehemu kilianza na safari ya Yosefu na Maria aliyekuwa na baraka tumboni. Walienda huko kwa ajili ya senza. Katika pilikapilika za kutafuta mahali pa kulala mama akajifungua mtoto wake hapo Betlehemu mji wa Daudi (Lk. 2:4). Baada ya kuzaliwa, mtoto huyo akaviringishwa nguo za mtoto mchanga na kulazwa kwenye hori la kulishilia wanyama.

Hii ndiyo alama ambayo malaika waliwapa maelezo wachungaji na kuwaagiza waende huko kumwona mtoto. Malaika wakawaambia wachungaji: “Leo katika mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristu Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hoi ya kulia ng’ombe.”

Kumbe yawezekana malaika walikuwa wa kwanza kufika hapo Betlehemu na kushuhudia mambo yalivyo kabla ya kwenda kuwahabarisha wachungaji. Tunaambiwa pia kwamba mara tu baada ya malaika kuondoka, wachungaji nao wakaambizana wenyewe, Jamani tusiilazie damu taarifa hii ya malaika: “Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.” (Lk. 2:15). Baada ya kumwona mtoto wakaanza nao wakaanza kutawanya habari: “Walipomwona (mtoto Yesu) wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Halafu wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.” (Lk 2:27).

Malaika walipoona utukufu umetua Bethlehemu, hawakuuacha utulie tu pale pangoni, bali wakaondoka kwenda kuutangaza kwa wachungaji. Kwa hiyo utukufu haukuhusu pango ila unawahusu wachungaji wanaowakilisha wanyonge wote. Wachungaji ndiyo wanaodhihirisha utukufu wa Mungu. Mungu anajidhihirisha na kutukuzwa pale tu ambapo wanyonge, fukara wanapofurahi. Huo ni utukufu wa Mungu.
Wachungaji wanafurahi kwa sababu kutokana na hali halisi ya unyonge wao, walijisikia kama watu waliolaaniwa, kwa hiyo hawakutegemea kabisa kupata mawasiliano na Mungu. Kumbe amezaliwa mchungaji mwenzao, anayejua unyonge wao. Hawakujiamini wenyewe, na mara moja wakaanza kushauriana wenyewe na kuchukua maamuzi ya kwenda kushuhudia na baadaye kutoa ushuhuda.

“Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.” Wanaenda haraka, kushuhudia utukufu wa Mungu, ambao ni kutaka watu wapate furaha haraka. Kwetu sisi tungetegemea kusikia mambo ya ajabu zaidi au hata kusikia muujiza. Hakuna maelekezo zaidi, ni kama vile amezaliwa mtoto wa kawaida. Maisha ya kawaida yanaendelea. Yesu kuwa Mungu hakutegemei muujiza wa pekee, bali yeye mwenyewe jinsi alivyo. Yeye ni kama sisi, Mungu amekuwa mwenzetu. Anayemtegemea Mungu wa kufanya miujiza, ujue mungu aina hiyo ni mungu wa kipagani.

Wachungaji wanaenda Betlehemu na wanamwona mtoto aliyeviringishwa nguo. Hiyo ndiyo picha mpya ya Mungu anayejidhihirisha kwa binadamu. Watoto waliviringishwa nguo ili kuwakinga na baridi lakini pia inayo maana ya kidini. Mtoto ni safi, hivi huwezi kumshika tu kwa mikono, lakini kuna maana pia muhimu ya kiroho, hasa mwinjili anaposisitiza jinsi mtoto alivyoviringishwa nguo, hoja kubwa ni kusudi mtoto huyo aweze kuguswa, kushikwashikwa na kubebwa na watu wote.

Aidha imeandikwa mara tatu kuwa aliwekwa katika hori la kulishia chakula wanyama (ng’ombe). Kwa hiyo msisitizo huo unahusu chakula. Mtoto aliviringishwa nguo, kama vile mkate unavyoviringishwa karatasi au majani na kuwekwa kwenye nyumba ya mkate (Bethlehemu). Kwamba Yesu anadhihirishwa hapa kama mkate yaani chakula. Malaika wanawaelekeza wachungaji kwenda kwenye nyumba ya mkate (bethlehemu) huko watauona mkate umeviringishwa.

“Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hoi ya kulia ng’ombe.”Yesu aliishi na kuhitimisha historia ya maisha yake hapa duniani akijionesha mwenyewe daima kuwa ni mkate utokao mbinguni. Maisha yake yote akayatolea hadi chembe ya mwisho ya mkate. “Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.”

Wachungaji wanapofika pangoni wakamwona Maria, Yosefu na mtoto mchanga amelala horini. Hawaoni cha pekee zaidi. Kisha wakatoa taarifa juu ya kile walichoambiwa juu ya huyo mtoto. “Walipomwona (mtoto Yesu) wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Halafu wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.” Nadhani watu wote walishangazwa na taarifa hizo kwani ni Mungu aina gani anayeweza kuwatokea watu wanyonge kama wachungaji. Kama ndivyo basi hayo ni maajabu.

Tunaambiwa jambo jingine lililotokea pale Bethlehemu ni kuwa Maria akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Neno kufikiri, siyo tafsiri sahihi, kwa kigiriki “sinmbalus” inamanisha kuweka mambo pamoja na kutafakari, hasa kule ambako mmoja unapoona mambo lakini unashindwa kuyaelewa. Maria anatulia, anaangalia, anaunganisha mambo anaweka pamoja mambo yanayomtukia. Atakuja kufahamu atakapokuwa amesimama chini ya Msalaba.

Wachungaji wanaondoka wakimshukuru na kumsifu Mungu – wameyaona maisha mapya. Wamemwona Mungu aliyejifanya binadamu na kulingana na watu. Wamemwona Mungu anayejiacha kushikwashikwa na watu wenye mikono michafu, watu wanaonuka, yaani wanyonge, maskini, wazee, wenye dhambi, walalahoi. Watu hawa wanyonge wameona na wanafurahi, wanamshukuru na kumsifu Mungu, kisha wanamshuhudia.

Kumbe, watu hawa wanyonge tu ndiyo wanaoweza kutambua na kushabikia sera hii kubwa ya Mungu kujifanya mtu. Ni watu kama hawa ndiyo wanaoweza kuwa na furaha, na kusifu na kumshukuru Mungu. Kwa wataalamu, wakuu, matajiri sera hii haiingii akili na mioyoni mwao.

Ni muhimu hata kwetu kwamba badala ya kujihoji na kufikri nini tufanye nini katika maisha, baada ya kumwona Kristu tubaki tu kufurahi. Tumeona tendo kuu la upendo alilotufanyia Mungu. Huo ndiyo mwanzo wa uchumba kati ya Mungu na binadamu, kati ya Yesu na Kanisa lake. Sisi tunafunganishwa na Yesu katika upendo. Ndiyo mwanzo wa maisha ya upendo na ya furaha. Wanaopendana daima wanashika simu mkononi wakisubiri ”message au kupib”, au kuitwa na mpendwa wao ili kuongeana.

Sisi tukitaka kugundua utukufu na upendo huo wa Mungu tuanza Bethlehemu, na kuendelea mbele hadi kwenye majitoleo kamili ya Yesu kule Kalvari. Kwa hiyo ndugu zangu “twendeni na Papa mpaka Betlehemu” tukirudi toka huko tuwapagawaze watu kwa tutakayoyaona. Hebu sasa tutoke Bethlehemu kuongozane na Papa hadi mto Yordani.

Imeandaliwa na
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.