2014-05-14 07:21:04

Familia ni shule makini ya Injili ya maisha!


Maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa, kutunzwa na kuendelezwa kwani ni msingi wa haki zote za binadamu. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, walioshiriki katika maandamano makubwa nchini Canada, kama sehemu ya mchakato wa kutetea zawadi ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na maadhimisho ya Juma la Familia nchini Canada.

Katika ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema anapenda kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika kulinda, kutetea na kuendeleza Injili ya Uhai. Maandamano haya ni chachu inayopania kuamsha dhamiri nyofu miongoni mwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukumbatia na kuenzi Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi Mungu. Watoto wanapaswa kulindwa kisheria kwani hii ni haki yao msingi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika kipindi cha miaka kumi na saba, limekuwa likiadhimisha Juma la Familia kila mwaka kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 18 Mei ili kushiriki pia katika Siku ya Familia Kimataifa, inayoadhimishwa na Umoja wa Mataifa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Mei. Maadhimisho haya ni sehemu ya mkakati wa kichungaji uliobuniwa na Maaskofu ili kuwajengea watu msingi wa kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha na tunu msingi za ndoa na familia nchini Canada.

Dhana hii imefanyiwa kazi kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliopania kuwapatia waamini nafasi ya kuifahamu imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; imani inayoadhimishwa katika Sakramenti za Kanisa, Imani inayomwilishwa katika Amri za Mungu na Imani inayojionesha katika sala.

Maadhimisho ya Juma la Familia nchini Canada kwa mwaka 2014 yanaongozwa na kauli mbiu "Familia zikiwa zimeungana katika furaha ya Kristo". Tema hii imechaguliwa kutokana na tukio la Mama Kanisa kuwatangaza watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II, viongozi wa Kanisa waliosimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; utu na heshima ya binadamu. Huu ndio mwendelezo wa mikakati ya kichungaji unaofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, ili kukabiliana na changamoto za maisha ya ndoa na familia ameitisha Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014.

Baraza la Maaskofu Canada linasema, kuna uhusiano wa dhati kati ya Familia na Maisha, kwani familia ni chemchemi ya maisha na wao ndio wenye dhamana na jukumu la msingi kuhakikisha kwamba, zawadi ya maisha inaendelezwa hata pale wanapokabiliana na changamoto za maisha. Familia ni shule makini ya maisha na kwamba, maisha ya binadamu hayana mbadala! Familia ya Kikristo ina dhamana ya kuhakikisha kwamba, inarithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni.







All the contents on this site are copyrighted ©.