Patriaki Fouad Twal wa Yerusalemu ni kati ya wageni mashuhuri walioshiriki katika
mkesha na maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka tisini na saba, tangu Bikira Maria alipowatokea
Watoto wa Fatima: Yacinta, Francis na Lucia; Siku kuu ambayo inaadhimishwa na Mama
Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 13 Mei. Ni siku ambayo, watu wengi wanakumbuka,
jaribio la kutaka kumuua Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.
Patriaki Twal amewataka
waamini kusali kwa ajili ya kuombea haki na amani huko Mashariki ya Kati pamoja na
kuendelea kuwasaidia kwa hali na mali pamoja na kuhakikisha kwamba, sheria za kimataifa
zinaheshimiwa na kutekelezwa huko Mashariki ya kati kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya wengi. Patriaki Twal anasema, nia yake ni kumwomba Bikira Maria wa Fatima, ili
aweze kusaidia kufanikisha hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko huko Mashariki
ya Kati, inayoongozwa na kauli mbiu, ili wote wawe wamoja, itakayoanza hapo tarehe
24 hadi tarehe 26 Mei 2014. Hapa Baba Mtakatifu anatarajiwa kutembelea Yordan, Palestina
na Israeli.
Patriaki Twal amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema
kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kichungaji na kiekumene
huko Mashariki ya Kati, huko ni mahali ambapo Ukristo umeota mizizi inayoonesha historia
nzima ya Ukombozi.