Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayoweza kupokelewa na mwamini akiwa ameungana na
Mwenyezi Mungu pamoja na Kanisa lake na kwamba, madhulumu ndani ya Kanisa yamewawezesha
waamini kuwa jasiri na hivyo kutoka kifua mbele kutangaza Habari Njema ya Wokovu kati
ya mataifa, huko Antiokia na Ugiriki, watu wakamfungulia Kristo malango ya maisha
yao na wengi wakabatizwa!
Ni kundi la waamini lililojiachilia mikononi mwa
Roho Mtakatifu, ili aweze kutenda kadiri ya uwezo wake, hii ndiyo nguvu ya Roho Mtakatifu
inayoweza kutenda hadi kuwashangaza wengi, kama alivyofanya Filipo alipombatiza Malkia
wa kushi au Mtakatifu Petro aliyepelekwa kumbatiza Korneli na familia yake, changamoto
na mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Roho Mtakatifu bila kumwekea kizingiti, bali
kujivika fadhila ya unyenyekevu.
Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba
Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko
mjini Vatican siku ya Jumanne, tarehe 13 Mei 2014. Baba Mtakatifu anasema kuna kundi
la Wakuu wa Makuhani ambalo daima lilikuwa linasigana na Yesu katika mambo mengi,
kwani wao walidhani kwamba, dini ilijisimika katika Sheria na kile ambacho wao waliamini
kutoka akilini mwao, wakashindwa kutambua kwamba, walihitaji upendo na uzuri wa imani,
kwani hili ni kundi linalotaka maelezo basi!
Baba Mtakatifu anasema hawa ni
watu waliokuwa na shingo nguvu, hata baada ya kupewa maelezo ya kina na Yesu, bado
waliendelea kumfuata futa wakitaka kwanza kabisa kumnyamazisha na hatimaye kumfutilia
mbali kutoka katika uso wa dunia. Walishindwa kufungua mioyo yao kwa Mtakatifu wa
Mungu na kwa Roho Mtakatifu. Ni watu waliokuwa na kiburi na kujiamini kupita kiasi,
ni watu ambao hawakupenda kuwa sehemu ya kundi la Kondoo wa Kristo, kwani walifunga
kabisa mioyo yao.
Imani ni zawadi inayopokelewa na mtu binafsi na kuendelea
kuiboresha kwa maisha ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kushikamana na watu wa Mungu
wanaofanya hija ya imani kwa kusikiliza kwa unyofu, kile ambacho Roho Mtakatifu anataka
kutoka kwa Kanisa. Kiburi na majivuno anasema Baba Mtakatifu ni hatari kwa ustawi
wa maisha ya kiroho, mwaliko kwa waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia
kuwa wasikivu na wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu na kutekeleza kile anacho waambia.