Serikali ya Mauritius hivi karibuni imeanza mchakato wa mabadiliko ya kuandika Katiba
Mpya na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini humo linasema, Katiba mpya haina budi kuwapatia
wananchi wa Mauritius utu na heshima ya kidemokrasia. Maaskofu wamepongeza rasimu
ya Katiba mpya kwa kuondoa harufu ya ukabila ndani ya Katiba, jambo ambalo ni sumu
na kikwazo cha maendeleo endelevu wakati wa kupiga kura.
Askofu mkuu
Maurice Piat wa Jimbo Katoliki la Port-Louis anasema, pamoja na hatua hii ambayo imefikiwa
na Serikali ya Mauritius kwa sasa lakini bado kuna haja ya kujenga na kuimarisha umoja
na mshikamano wa kitaifa, kwa kuhakikisha kwamba, wabunge wanaochaguliwa na wananchi
wanawakilisha maoni, matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao
ya kila siku.
Kwa sasa wananchi wengi hawana imani na wabunge wao kutokana
na kujikita mno katika ubinafsi na kusahau mafao ya wengi, mambo ambayo yanaweza kuchangia
kusuasua kwa mchakato wa kukuza na kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria nchini
humo.
Uwakilishi wa wanawake ndani ya Bunge ni kati ya mabadiliko makubwa yanayooneshwa
kwenye Muswada wa Katiba Mpya, ili kuleta uwiano na ubora katika mijadala mbali mbali
ndani ya Bunge kwa kuwashirikisha wanawake katika kuchangia na kutoa maamuzi katika
ustawi na maendeleo ya wengi.
Maaskofu wanapongeza pia mchango wa Tume huru
ya uchaguzi katika kupanga na kuteua wabunge kufuatana na vipaumbele vya majina kutoka
katika vyama husika. Jambo muhimu la kuzingatia ni kuhakikisha kwamba, Tume huru ya
uchaguzi inatekeleza dhamana yake kwa kuzingatia kanuni msingi za ukweli, uwazi na
mafao ya wengi, kama njia ya kufutilia mbali rushwa na ufisadi ambao umekuwa ni sumu
ya demokrasia ya kweli. Ili kukuza haki msingi za binadamu, utawala wa sheria, mafao
ya wengi na amani ya kudumu, viongozi wa kisiasa hawana budi kutafuta mwarobaini wa
matatizo na changamoto zilizoko nchini mwao ili kutibu kuanzia kwenye mizizi yake.
Rasilimali ya nchi haina budi kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya
wananchi wote na wala si kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache wenye uchu wa mali
na madaraka. Katiba Mpya iwe kweli ni sheria mama itakayorudisha hadhi na demokrasia
ya kweli nchini Mauritius.