Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, mahubiri yanayotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko walau kila siku wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa
Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican ni chachu ya
mageuzi katika mchakato wa mawasiliano ndani ya Kanisa, unaofanywa na Baba Mtakatifu
Francisko kwa wakati huu.
Padre Lombardi ameyasema hayo wakati anashiriki katika
mjadala kuhusu mageuzi katika nyanja za mawasiliano yanayoendelea kuletwa na Baba
Mtakatifu Francisko, ulioandaliwa kwenye Onesho la Vitabu Kimataifa mjini Torino,
Kaskazini mwa Italia, mwishoni mwa Juma na Vatican kushiriki kama mgeni wa heshima.
Mahubiri ya Baba Mtakatifu yanawalenga wote wanaotaka kusikiliza Kanisa linasema
nini katika maisha yake ya kila siku kadiri ya Neno la Mungu na Maadhimisho ya Fumbo
la Ekaristi Takatifu. Huu nimwelekeo mpya wa mawasiliano ndani ya Kanisa na Jamii
katika ujumla wake.
Ni kiongozi anayegusa wengi kwa mtindo wake wa maisha
na jinsi anavyozungumza kwa kugusa undani wa maisha ya mwanadamu, kwake, mawasiliano
ni njia mahususi inayomwezesha mtu kukutana na jirani zake, ili kujenga umoja na mshikamano.
Baba Mtakatifu ni kinara wa mawasiliano katika masuala ya imani katika mitandao ya
mawasiliano kijamii.
Baba Mtakatifu Francisko anajitahidi kushirikisha mang'amuzi
na uzoefu wake kwa kukutana na kuzungumza na watu, kwa njia ya mahubiri na hotuba
zake mbali mbali.