Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha
kilichoko mjini Vatican, Jumatatu tarehe 12 Mei 2014 anasema kwamba, wapagani waliomwongokea
Kristo ilikuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kusonga mbele katika
maisha na utume wake na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kuzuia nguvu ya Roho
Mtakatifu, kwani Roho Mtakatifu anavuma pale anapotaka.
Baba Mtakatifu anasema
kishawishi kikubwa kwa baadhi ya waamini ni kutaka kumwongoza Roho Mtakatifu kadiri
ya vionjo na nia zao. Hiki ni kishawishi ambacho kimekuwepo hata ndani ya Kanisa kama
inavyojionesha katika Liturujia ya Neno la Mungu katika Kitabu cha Matendo ya Mitume.
Jumuiya ya Wapagani inapokea Neno la Mungu na Mtakatifu Petro ni shahidi wa ujio wa
Roho Mtakatifu kwa watu hawa waliomwongokea Kristo. Kwa bahati mbaya anasema Baba
Mtakatifu kuna baadhi ya watu waliotaka bado kushikilia Mapokeo na tamaduni zao za
awali, kwao hii inakuwa ni kashfa ya mwaka!
Mtakatifu Petro alifafanua jinsi
ambavyo Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo alivyowajalia wapagani zawadi ya
wokovu kwa njia ya wongofu wa ndani, kumbe, hakuna na sababu yoyote ya kumzuia Roho
Mtakatifu kutenda kazi yake. Kwa maneno haya ya hekima na busara, amani na utulivu
vinarejea tena katika Jumuiya ya Wakristo wa kwanza.
Baba Mtakatifu anawataka
waamini kutomwekea Roho Mtakatifu kizingiti anapowaonesha waja wake njia ya kufuata,
changamoto na mwaliko kwa Maaskofu na Mapadre kuwa na ujasiri wa kumwachia nafasi
Roho Mtakatifu katika maamuzi yao. Wawe ni wahudumu wanaomfungulia Roho Mtakatifu
mlango na kamwe wasimfungie nje, kwani Kanisa linaendelea kusonga mbele kutokana na
uwepo wa Roho Mtakatifu, anayewafundisha ukweli wote!
Baba Mtakatifu anasema,
Roho Mtakatifu ni kielelezo hai cha uwepo wa Mungu ndani ya Kanisa na nguvu inayolisukuma
Kanisa kusonga mbele katika maisha na utume wake. Roho Mtakatifu na karama zake, analiongoza
Kanisa na kwamba, huwezi kulifahamu Kanisa kwa ukamilifu bila ya uwepo wa Roho Mtakatifu.
Ni Roho Mtakatifu anayefanya mageuzi ndani ya Kanisa kama alivyosema Mtakatifu Yohane
XXIII.
Ni wajibu wa waamini kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie unyenyekevu
wa kuweza kusikiliza na kuelewa kile anachozungumza kwa ajili ya Kanisa kutoka katika
undani wa mioyo ya watu. Roho Mtakatifu anatumia nafasi na matukio mbali mbali kuzungumza
na Kanisa.