Baraza la Maaskofu Katoliki Chile katika mkutano wake wa 107 uliofunguliwa hapo tarehe
5 na kuhitimishwa tarehe 10 Mei 2014, limejadili kwa kina na mapana kuhusu hali ya
miito ya Kipadre na Kitawa pamoja na kuangalia hali ya Seminari zake, kama sehemu
ya mkakati mkubwa wa maboresho unaopaniwa kutekelezwa na Maaskofu nchini Chile, kwa
ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Imekuwa ni fursa ya kuangalia hali ya Chile
katika ujumla wake.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Chile linasema, kuna haja kwa waamini kutolea ushuhuda angavu wa
maisha yanayojikita katika imani, maadili na utu wema, ili kuwaonjesha wale wasioamini
umuhimu wa kukutana, kutembea na kumkubali Yesu kuwa ni Mwalimu na Bwana katika maisha.
Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Askofu mkuu Ivo Scapolo, Balozi wa Vatican nchini
Chile katika hotuba yake ya ufunguzi ambayo pia aliwasilisha salam na matashi mema
kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maaskofu hawa.
Maaskofu wameangalia
pia utekelezaji wa Mpango wa shughuli za kichungaji nchini Chile kuanzia Mwaka 2014
hadi Mwaka 2020, unaoongozwa na kauli mbiu “Kanisa linalosikiliza, linalotangaza na
kuenzi”. Maaskofu pia wamepembua kwa kina na mapana changamoto mbali mbali zinazojitokeza
katika maisha na utume wa Kanisa hususan kuhusu: Mihimili mikuu ya Uinjilishaji, Elimu,
Mikakati ya kichungaji katika masuala ya kijamii; Huduma na Mawasiliano.
Mkutano
huu umefungwa kwa Ibada ya Misa Takatifu ya kuwaweka wakfu Maaskofu wapya wasaidizi
wa Jimbo kuu la Santiago. Hawa ni: Askofu Fernando Ramos na Askofu Galo Fernandes.