2014-05-11 10:27:25

Rushwa ni saratani ya Jamii mamboleo!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni pamoja na Padre Antonio Spadaro, mkurugenzi mkuu wa Jarida la "Civiltà Cattolica" wameshiriki kujibu maswali ya waandishi wa habari Jumamosi, 10 Mei 2014 katika Onesho la Vitabu Kimataifa mjini Torino, Kaskazini mwa Italia.

Kimsingi wamezungumzia kuhusu mchakato wa mawasiliano unaofanywa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na azma yake ya kutaka kufanya mabadiliko makubwa katika Sekretarieti ya Vatican mintarafu ushauri uliotolewa na Makardinali wakati wa mikutano yao elekezi.

Anasema, Jamii nyingi zinaendelea kukumbwa na saratani ya rushwa inayopenyeza mizizi yake katika medani mbali mbali za maisha, kumbe kuna haja kwa Jamii kuendelea kuwa macho na makini kupambana kufa na kupona na vitendo vya rushwa vinavyodhalilisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Mabadiliko yanayotekelezwa na Baba Mtakatifu ni kuhakikisha kwamba, Sektretarieti ya Vatican inatekeleza dhamana yake kadiri ya mahitaji ya Kanisa la Kiulimwengu, kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma.

Licha ya watu kutumia diplomasia na mbinu mbali mbali za uongozi, lakini Baba Mtakatifu Francisko ameamsha dhamiri za watu, anaendelea kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo thabiti, licha ya magumu na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza duniani.

Kardinali Parolin anasema, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014 ina mwelekeo wa kiekumene, ni hija ya sala na tafakari kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Hija hii pia inagusa masuala ya kisiasa.

Ni matumaini ya Vatican kwamba, Israeli na Palestina wataendelea na majadiliano ya amani. Kuna haja ya kuendeleza juhudi za kusitisha vita na kujikita katika amani na upatanisho wa kitaifa nchini Syria, ambako kuna idadi kubwa ya watu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita. Vita ni chanzo kikuu cha mateso ya watu, kumbe kuna haja ya kuanzisha mchakato mpya unaojikita katika majadiliano ya kweli, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Kardinali Gianfranco Ravasi anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake anaendelea kutoa changamoto kubwa katika masuala ya mawasiliano ya kijamii, kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa watu kukutana, kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama ndugu.

Padre Antonio Spadaro anasema, katika onesho la vitabu kimataifa huko Torino, watu wengi wameonesha kiu na hamu ya kutaka kununua na kujisomea vitabu vya maisha ya kiroho. Huu ndio mwelekeo wa soko la vitabu vingi vinavyouzika sokoni. Kumbe, ushiriki wa Vatican katika onesho hili ni kutaka kuzima kiu ya watu katika maisha ya kiroho kwa kuwapatia vitabu vile ambavyo roho inapenda. Watu wanapenda kumsikiliza Papa Francisko kwani ni kiongozi anayezungumza mambo yanayogusa undani wa mtu katika Jamii mamboleo.







All the contents on this site are copyrighted ©.