2014-05-11 15:06:55

Onesheni sura ya Kristo mchungaji mwema!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 11 Mei 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kutoa Daraja Takatifu la Upadre kwa Mashemasi kumi na watatu kutoka Jimbo kuu la Roma. Mapadre hawa wanaitwa kushiriki Ukuhani wa Kristo aliouanzisha kwa njia ya Agano Jipya. Akaamua kati ya wafuasi wake, kuchagua baadhi kuwa ni Mitume, ili waendeleze utume wake binafsi kama Mwalimu, Kuhani na Mchungaji.

Mashemasi hawa wamefikia uamuzi uliofanywa katika ukomavu, ili kujitoa kwa ajili ya huduma kwa Kristo: Mwalimu, Kuhani na Mchungaji kwa kushirikiana kwa dhati katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa miongoni mwa Familia ya Mungu, Hekalu la Roho Mtakatifu. Mashemasi hawa wamewekwa wakfu ili wafanane na Makuhani wa Agano Jipya kwa kuungana na Maaskofu wao mahalia, ili kutangaza Injili na kuwachunga Watu wa Mungu pamoja na kushiriki katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na hasa zaidi katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu amewakumbusha Mapadre wateule kwamba, wanashiriki utume wa Kristo, Bwana na Mwalimu kwa kufundisha Neno la Mungu ambalo wao wenyewe wamelipokea kwa furaha kutoka kwa walezi wao. Huu ni mwaliko wa kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha katika imani tendaji: Wanapaswa kuwa waaminifu kwa Mafundisho ya Kristo ili kuwamegea Watu wa Mungu ile furaha na ushuhuda wa maisha yanayolijenga Kanisa la Mungu.

Kama Mapadre wataendeleza kazi ya kuwatakatifuza Watu wa Mungu na kutolea Sadaka takatifu ya Fumbo la Pasaka linaloadhimishwa kila siku Altareni. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, watalijalia Kanisa watoto wapya, kwa Sakramenti ya Upatanisho, watawaondolea waamini dhambi zao kwa kuwaonjesha huruma na upendo wa Kristo, jambo ambalo wanapaswa kulipatia kipaumbele cha kwanza. Wawajengee watu ari na moyo wa kukimbilia kwenye kiti cha huruma kwa ajili ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, watu wanaingia kwa Kristo ambaye ni mlango wa huruma.

Kwa njia ya Mpako wa wagonjwa, watawasaidia na kuwaombea wamini wagonjwa katika shida na mahangaiko yao kwa njia ya Sala ya Kanisa, watakuwa ni sauti ya Watu wa Mungu na kwa ajili ya ulimwengu mzima. Mapadre watambue kwamba, wameteuliwa kati ya watu kwa ajili ya mambo ya Mungu, mwaliko wa kutekeleza utume huu kwa furaha na upendo kadiri ya mapenzi ya Mungu na wala si kwa ajili ya kuridhisha matakwa yao! Mapadre wajitahidi kuwa kweli ni wachungaji wema.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawakumbusha Mapadre wapya kwamba, kwa kushiriki utume wa Kristo wakiwa wameungana na Askofu wao mahalia, wajitaabishe kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo, ili waweze kuwapeleka wote kwenye Fumbo la Utatu Mtakatifu. Daima mbele yao wawe na sura ya Kristo Mchungaji mwema aliyekuja si kwa ajili ya kuhudumiwa bali kuhudumia na kutoa maisha yake ili kuokoa wale waliokuwa wamepotea!







All the contents on this site are copyrighted ©.