2014-05-11 09:05:51

Msikubali kupokwa upendo wa shule!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni, tarehe 10 Mei 2014 amewashukuru wadau mbali mbali waliofanikisha maadhimisho ya Siku kuu ya Shule nchini Italia, iliyowawezesha maelfu ya wanafunzi, wazazi, walimu na wafanyakazi katika sekta ya elimu kumiminika kwa wingi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kuonesha umuhimu wa shule katika majiundi ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anatambua matatizo na changamoto zilizoko kwenye sekta ya elimu nchini Italia, kumbe, siku hii haikuwa ni kwa ajili ya kulalama, bali kuonesha kwamba, watu bado wanapenda shule na kwamba, hata Yeye binafsi anapenda shule, urithi aliomwachia mwalimu wake aliyemfundisha tangu akiwa mdogo, akaendelea na mwelekeo huo kama Padre, Askofu na sasa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, anapenda shule kwani hapa ni mahali pa wazi panapomonesha mtu ukweli, kwa kumfungua akili na moyo wake ili kutambua ukweli na mwelekeo mpya pamoja na utajiri wake wote. Ni mahali ambapo mwanafunzi anapata mbinu na mikakati ya kujifunza mambo mbali mbali ambayo yataendelea kuwa ni sehemu ya urithi wake hata kwa siku za usoni. Shule kimsingi ni mahali pa mtu anajifunza kufundishwa. Walimu ni kundi la kwanza linalopaswa kuwa wazi katika mchakato wa kujifunza ukweli na uhalisia wa mambo, kwa mwalimu ambaye hawezi kujiendeleza huyo ni mzigo!

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, anapenda shule kwani hapa ni mahali pa watu kukutanika na kuanza kutembea kwa pamoja. Jamii inahitaji kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana, ili kufahamiana, kupendana na kusaidiana. Shule ni muhimu sana katika ukuaji wa mtu mzima na ukamilifu wa dhamana inayotekelezwa na Familia. Hapa ni mahali pa kujenga mahusiano ya kijamii, kumbe, familia na shule ni chanda na pete, zinategemeana, shirikiana na kukamilishana, kwani kama wanavyosema wahenga kutoka Afrika kwamba, "Kumwelimisha mtoto kunahitaji kijiji kizima". Kumwelimisha kijana kunahitaji wadau mbali mbali ambao kila mtu anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake.

Baba Mtakatifu anasema anapenda shule kwa sababu ni mahali panapofundisha: ukweli, wema na uzuri. Ikumbukwe kwamba, ni vyema kushindwa kwa uhalali, kuliko kupata ushindi kutokana na mchezo mchafu! Ni dhamana ya shule kukuza na kuendeleza kilicho kweli, chema na kizuri, ili kuweza kuifunda akili, dhamiri na mahusiano, mambo yanayotegemeana na kumsaidia mtu kupenda na kuthamini zawadi ya maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kuteta kwamba, shule ni mahali ambapo watu wanajifunza tabia na tunu msingi za maisha: kiroho na kimwili. Hapa mtu anajifunza kufahamu mambo mengi, ili kujenga na kukuza tabia yake inayopaswa kujikita katika tunu msingi za maisha. Baba Mtakatifu anawatakia kheri na fanaka wanafunzi, wazazi, walimu na wafanyakazi katika sekta ya elimu, kuendeleza safari hii inayowawezesha watu kukua na kukomaa: kwa kusema, kufikiri na kutenda. Mwishoni kabisa baba Mtakatifu amewaambia watu kwamba, kamwe wasikubali kupokonywa upendo wao kwa shule!







All the contents on this site are copyrighted ©.