Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Jumamosi, tarehe 10 Mei 2014 limeadhimisha Siku
kuu ya shule nchini Italia kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Zaidi ya watu laki tatu walifurika
kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro na viunga vyake kushudia kwa mara nyingine tena,
Kanisa likihimiza umuhimu wa shule kama hija ya majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili,
dhana ambayo vijana wa kizazi kipya wanapaswa kurithishwa kwa ukamilifu zaidi.
Tukio
hili limewawezesha watu kusikia shuhuda mbali mbali zilizotolewa na watu maarufu kutoka
Italia jinsi ambavyo wameweza kufanikiwa katika maisha yao kwa kukazia: umuhimu wa
mtu kujiwekea malengo katika maisha na kujisadaka ili kuweza kufanikisha malengo haya
kwa kutambua kwamba, katika maisha hakuna njia ya mkato na kama ipo, hiyo ni njia
itakayomwachia mtu madonda ya kudumu. Kuna haja ya kukazia tunu msingi za maisha ya
kiroho na kimwili; uaminifu, ukweli, uwazi na udumifu pamoja na kuwa na matumizi sahihi
ya vyombo vya habari kama mahali pa kukutana na watu ili kujiendeleza zaidi.
Kardinali
Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema kwamba, sekta
ya elimu nchini Italia inakabiliwa na matatizo makubwa yanayojikita katika miundo
mbinu, hali ambayo wakati mwingine inakatisha tamaa. Lakini ikumbukwe kwamba, shule
ni mahali ambapo mtu anafundwa kuwa na upembuzi yakinifu katika maisha yake; kwa kutambua
kanuni maadili pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa mawazo mbali mbali yanayoendelea
kujitokeza. Hapa ni mahali ambapo wanafunzi wanapaswa kutafuta na kupata ukweli, wema
na uzuri.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika mikakati yake ya kichungaji
kwa kipindi cha miaka kumi, linatoa kipaumbele cha kwanza katika sekta ya elimu kama
sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji, ili kuwawezesha waamini kufanya mageuzi ya ndani,
kwa kujenga utamaduni wa kukutana na kuthaminiana ili hatimaye kutambua ukweli. Kanisa
Katoliki nchini Italia limechangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya
elimu, ndiyo maana linaendelea kutoa changamoto ya kuwekeza zaidi katika sekta ya
elimu kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya, kwani hii ni haki yao msingi.
Kardinali
Bagnasco anasema, wazazi wanayo haki ya kuchagua mfumo na mahali ambapo watoto wao
wanaweza kupata elimu bora zaidi, kama inavyobainishwa na Katiba ya nchi. Baraza la
Maaskofu Katoliki Italia linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwasaidia waamini
kukua kiumri, hekima na neema, inayobubujika kutoka katika kweli za Kiinjili.
Naye
Waziri wa Elimu nchini Italia Bibi Stefania Giannini anasema, kwake tukio hili halitaweza
kufutika kwa urahisi moyoni mwake, kupata nafasi ya kuzungumza mbele ya Baba Mtakatifu
pamoja na kusikilizwa na umati mkubwa wa watu uliokuwa umefurika kwenye Uwanja wa
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro.
Hii inaonesha kwamba, kuna haja ya kuwaelimisha
wanafunzi kutambua na kuheshimu umuhimu wa shule na kazi na kwamba, shule uwe ni mfumo
unaowashirikisha wengi. Shule ni kwa ajili ya mafao ya wengi, changamoto ya kuendeleza
mshikamano wa dhati pamoja na kuongeza rasilimali watu na fedha ili kufanikisha mikakati
ya elimu.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni alitumia dakika 45 kuzunguka
na kuzungumza na wanafunzi, wazazi na waalimu waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Katika hotuba yake, ameonesha mambo makuu matatu yanayomfanya
kupenda shule: yaani shule inamwezesha mtu kuuona ukweli; ni mahali pa kukutana na
kwamba, hapa ni mahali ambapo mtu anafundwa kufahamu kilicho kweli, chema na kizuri.
Baba Mtakatifu mwishoni, alitumia fursa hii kusalimiana na wanafunzi na walimu
wagonjwa na baadaye akarudi kwenda kijipumzisha baada ya pilika pilika za siku nzima!