Familia ya Mungu inawajibika kukuza na kuendeleza miito!
Baba Mtakatifu katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malkia wa mbingu, Jumapili ya
Kristo mchungaji mwema sanjari na maadhimisho ya siku ya 51 ya kuombea miito mitakatifu
anasema, Yesu Kristo ndiye mchungaji mwema anayeonesha upole, unyenyekevu, ufahamu;
kiongozi anayethubutu kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kondoo wake, ili waweze
kupata utimilifu wa maisha. Huu ndio uhusiano unaopaswa kuoneshwa kati ya Wakristo
na kama kielelezo cha mahusiano ya kibinadamu.
Yesu Kristo ndiye mchungaji
wa kweli, anayewakirimia waja wake utimilifu wa maisha, mwaliko kwa kila mwamini kuwa
na imani kwa Kristo anayewaongoza, kwa kumsikiliza wakati anapozungumza nao kutoka
katika dhamiri zao nyofu, daima mioyo yao ikiwa wazi tayari kusikiliza Neno lake,
ili kulisha imani na kuangazia dhamiri zao, ili hatimaye, waweze kufuata mafundisho
yake kikamilifu.
Baba Mtakatifu anasema, kwa namna ya pekee, waamini wanaalikwa
kusali kwa ajili ya kuwambea Mapadre wapya kumi na watatu waliopadrishwa siku ya Jumapili,
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili waweze kuwa kweli ni waaminifu
kwa Kristo Mwalimu na viongozi wenye hekima na angavu kwa watu wa Mungu waliokabidhiwa
kwao. Wajitahidi kumwiga Kristo anayewaonesha njia na matumaini kwa watu wake, ili
aweze kuwa karibu zaidi kwa watu wake kwa njia ya huruma pamoja na kuwasaidia wale
waliochoka na kudhohofu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Kanisa linaadhimisha
Siku ya 51 ya Kuombea Miito mitakatifu, changamoto ya kila mtu kutoka katika ubinafsi
wake, ili kujiunga na Yesu pamoja na Injili yake, kwa kumfuasa Kristo katika furaha
sanjari na kutekeleza dhamana waliyokabidhiwa na Mama Kanisa, ili kujenga urafiki
wa dhati na kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza.
Baba Mtakatifu anawaalika
waamini kusali zaidi katika nyakati hizi ambamo sauti ya Kristo Mchungaji mwema inafifishwa
na kwamba, Familia ya Mungu iwajibike zaidi katika kukuza na kuhamasisha miito mitakatifu,
kwa kufahamu na kujiamini. Baba Mtakatifu amewaweka wote chini ya ulinzi na usimamizi
wa Bikira Maria, ili aweze kuendelea kuhamasisha miito mbali mbali ndani ya Kanisa