Wajengeni watu katika umoja, utakatifu na mapendo!
Hija ya kitume inayofanywa na Maaskofu mahalia mjini Vatican inalenga pamoja na mambo
mengine kuimarisha umoja, upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni nafasi
ya kusali na kutafakari, ili kujenga na kuimarisha uhusiano wao na Yesu Kristo, kwa
ajili ya huduma ya Injili.
Ni wakati muafaka wa kufanya tathmini ya kina kuhusu
maisha na utume wa Kanisa nchini Eritrea na Ethiopia, kwa kujadili furaha na changamoto
katika maisha na utume wa Kanisa. Hata katika utofauti wa nchi kama unavyojionesha
kwa Eritrea na Ethiopia, lakini kwa pamoja wanabeba ndani mwao utajiri na huduma kwa
Kanisa moja la Kristo!
Maaskofu wanahamasishwa kutangaza Injili ya Kristo,
kwa kuwajenga na kuwaimarisha waamini katika utakatifu, umoja na mapendo. Ni mwaliko
wa kushirikiana kwa dhati kati ya Makanisa ya Mashariki na Magharibi kwa ajili ya
ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu inayowaka mapendo ya Kristo, jambo la kufurahisha
na kujivunia kwa Kanisa nchini Eritrea na Ethiopia.
Imani inayoendelea kustawi
na kushamiri katika nchi hizi ni matunda ya kazi za kimissionari, watu waliothubutu
kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu,
changamoto na mwaliko wa kuwa na ari pamoja na mwamko mpya wa shughuli za kimissionari,
ili kuwawezesha watu kuishi na kuadhimisha vyema imani yao!
Hii ni hotuba iliyotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko kwa Maaskofu kutoka Eritrea na Ethiopia, Ijumaa tarehe
9 Mei 2014 baada ya kuhitimisha hija yao ya kitume inayofanyika mjini Vatican walau
kila baada ya miaka mitano. Anasema, dhamana ya Uinjilishaji waliyokabidhiwa na Mama
Kanisa wanaitekeleza kwa kushirikiana na Mapadre wao ambao ni wasaidizi wao wa karibu,
Kanisa linawashukuru Mapadre na Wamissionari, kwa kazi kubwa ya kuhubiri, kuadhimisha
Sakramenti za Kanisa pamoja na utekelezaji wa matendo ya huruma, kama kielelezo cha
uwepo wa Kristo kati ya watu wake.
Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza Maaskofu
kujitaabisha katika malezi ya Majandokasisi wao, ili waweze kuwa kweli ni watakatifu
na watangazaji mahiri wa Neno la Mungu, hawana budi kuendelea kuinjilishwa, kwa kukazia
majiundo makini Seminarini; majiundo yanayomgusa mtu mzima, kiroho, kiakili na kichungaji;
ili Mapadre wawe ni watu wa sala, wanaojisomea pamoja na kujisadaka pamoja na Maaskofu
kuwaonesha kwamba, wanawajali na kuwathamini, kwa kuwa wakarimu katika kuwatekelezea
mahitaji yao msingi: kiroho, kimwili na majiundo endelevu; wao wenyewe wasaidiane
na kutaabikiana, ili kujenga na kuimarisha udugu, ili kutolea ushuhuda wa ufuasi wa
Kikristo!
Baba Mtakatifu analipongeza Kanisa Katoliki Eritrea na Ethiopia ambalo
ni matunda ya ushirikiano wa watu mbali mbali, waliojisadaka hata kujenga na kuimarisha
Jumuiya za Kanisa mahalia. Hawa ni wamissionari waliojitosa katika huduma kwenye sekta
ya elimu, afya na huduma za kichungaji, ili kuwaonesha sura ya Kristo kwa kuishi Injili.
Baba Mtakatifu anawashukuru wote hawa akiungana na Maaskofu wao pamoja na kuwahimiza
Maaskofu kuendelea kuwahudumia katika mahitaji ya kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu
anasema, dhamana ya Uinjilishaji ni kwa Wakristo wote, changamoto kwa Kanisa kuendelea
kutoa majiundo makini kwa Makatekista, Waamini walei, Vijana, ili waweze kujenga na
kuimarisha uhusiano wao na Kristo hasa pale wanapokabiliana na changamoto za maisha.
Baba Mtakatifu anawataka waamini walei kuwasaidia vijana kufanya maamuzi makini kuhusu
maisha yao hasa kutokana na ukweli kwamba, fursa za ajira ni adimu kwa wengi. Kumbe,
kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana na viongozi walei ili waweze kutekeleza wajibu
wao barabara.
Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu pamoja na waamini walei kumtolea
Kristo ushuhuda makini, kwa kusaidia kupambana na umaskini ambao kwa kiasi kikubwa
ni matunda ya vita ya muda mrefu katika nchi hizi. Ushirikiano na wadau mbali mbali
unaweza kuleta nafuu kwa wananchi wengi, kwa watoto wanaokabiliana na utapiamlo wa
kutisha pamoja na watoto yatima.
Baba Mtakatifu anawakumbuka vijana wanaohatarisha
maisha yao kwa kufunga safari za hatari ili kutafuta maisha bora zaidi, lakini wawakumbuke
wazee wanaobaki nyumbani wakiteseka bila msaada. Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu
kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa ajili
ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wao.