Umoja wa Mataifa wamwalika Papa Francisko mjini New York!
Kwa niaba ya Familia ya binadamu wote, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon
amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 9 Mei 2014 kwa kuwapatia fursa
ya kuweza kuzungumza na wakurugenzi wakuu wa mashirika yanayosimamiwa na Umoja wa
Mataifa, waliokuwa wanafanya mkutano wao wa kupanga mikakati ya Umoja wa Mtaifa mjini
Roma.
Mkutano huu hufanyika mara mbili kwa mwaka ili kwa pamoja waweze kujadili
dhamana yao katika medani za kimataifa, kulinda amani pamoja na kuweka mikakati ya
maendeleo endelevu. Kama Familia ya Umoja wa Mataifa wanakabiliana na changamoto nyingi
kama vile: ongezeko kubwa la ukosefu wa usawa na haki; hali ya watu kutovumiliana
kwa misingi ya kidini pamoja na vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa wananchi
wanaoishi: Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Sudan ya Kusini, Syria na Ukraine ambako
hali bado ni tete sana!
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba, dunia
inaendelea kuguswa na athari za mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo itakuwa na madhara
makubwa kwa vizazi vijavyo, ndiyo maana Umoja wa Mataifa unaandaa mkutano wa kimataifa
utakaojadili kwa kina na mapana athari za mabadiliko ya tabianchi ili kuibua mbinu
mkakati wa kupambana na hatimaye, kudhibiti athari zake. Umoja wa Mataifa unaendelea
na kampeni yake ili kuhakikisha kwamba walau Malengo ya Maendeleo ya Millenia kwa
Mwaka 2015 yanafikiwa.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, hapa kunahitajika,
uvumilivu, ujasiri, ushirikiano pamoja na kuguswa na mahangaiko ya watu. Baba Mtakatifu
Francisko katika hotuba yake kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na wakurugenzi wa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa alisema kwamba, kanuni hizi msingi ni dira na mwongozo
wa watu wote. Umoja wa Mataifa unamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko
katika jitihada zake za kupambana na umaskini duniani kwa kujielekeza katika mikakati
ya maendeleo endelevu.
Umoja wa Mataifa anasema, Katibu mkuu una matumaini
makubwa na utaendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki katika kulinda na kudumisha
utu na heshima ya binadamu. Mwishoni, Bwana Ban Ki-Moon alitumia fursa hii kumkaribisha
rasmi Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York,
Marekani, kwani hii inaweza kuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kuweza kushirikisha mwono
na matumaini yake kwa binadamu.
Akigusia hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini
Korea, mahali alipozaliwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anasema
kwamba, ana matumaini kuwa Baba Mtakatifu atawapelekea ujumbe wa amani, utakaosaidia
kuponya na kuendeleza mchakato wa upatanisho kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya
Kusini.