Mwaka mmoja tangu Papa Tawadros II alipokutana na Baba Mtakatifu Francisko!
Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua ya shukrani Patriaki Tawadros II, wa Kanisa
la Kiorthodox la Alexandria, Misri, anapokumbuka mwaka mmoja tangu walipoonana mjini
Vatican tarehe 10 Mei 2013, kama kielelezo cha kuimarisha umoja na mshikamano kati
ya Makanisa, mchakato ulionzishwa na Papa Paulo VI pamoja na Papa Shenouda III kunako
mwaka 1973.
Katika barua hii Baba Mtakatifu Francisko anaangalia mchakato
wa upatanisho na urafiki ambao Makanisa haya yamefanya kwa pamoja. Kwa msaada wa Mwenyezi
Mungu wameendelea kufahamiana na hivyo kuvuka vizingiti vya kutoelewana vilivyojengeka
katika historia, kiasi kwamba Makanisa haya yanaanza kuonja cheche za umoja ambao
hata hivyo haujakamilika.
Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya majadiliano
katika upendo pamoja na uaminifu wataweza kumaliza tofauti ambazo bado ziko miongoni
mwao, ili kufikia umoja kamili. Baba Mtakatifu anakumbuka ile sala ya pamoja waliyosali
alipokuwa mjini Roma na kwamba, waendelee kusindikizana kwa njia ya sala kama watoto
wa Mungu, waliozaliwa katika Maji na Roho Mtakatifu na hivyo kupata mwanga wa imani,
ili wote wawe wamoja.
Baba Mtakatifu anapenda kumhakikishia Patriaki Tawadros
II sala zake kwa ajili ya Wakristo huko Misri na Mashariki ya Kati katika ujumla wake,
ili waweze kupata amani ya kudumu.