Daraja ni Sakramenti ambayo kwayo utume uliokabidhiwa na Kristo kwa mitume wake huendelea
kutekelezwa katika Kanisa hadi mwisho wa nyakati: hivyo hii ni Sakramenti ya huduma
ya kitume na ina ngazi tatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi. Hawa ni walimu wa Kanisa
wanaotekeleza dhamana yao katika utendaji wa kawaida wa Kanisa. Ushemasi ni ngazi
ya huduma.
Mababa wa
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba utimilifu wa Sakramenti ya Daraja
hutolewa kwa njia ya wakfu wa kiaskofu, ambao kimsingi ni ukuhani mkuu, yaani kilele
cha huduma takatifu. Askofu ana kazi kuu tatu: kuongoza, kutakasa na kuwafundisha
watu wa Mungu. Kwa maneno mengine, Askofu ni mwalimu, mchungaji na kuhani. Askofu
ana dhamana kwa Kanisa mahalia lakini pia anajishughulisha kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya Kanisa zima.
Fumbo la Ekaristi Takatifu linaloadhimishwa na Askofu
lina maana ya pekee kabisa kwani ni ishara ya Kanisa lililounganika kuizunguka Altare,
chini ya yule ambaye kwa namna inayoonekana anamwkilisha Kristo, Mchungaji Mwema na
Kichwa cha Kanisa lake.
Kwa tafakari hii inayoletwa kwako na Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican, inatupatia nafasi ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Askofu Moses
Hamungole wa Jimbo Katoliki Monze, Zambia, aliyewekwa wakfu na hatimaye kusimikwa
kuwa ni Askofu wa Monze hivi karibuni, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa
na Askofu mstaafu Emilio Patriarca wa Jimbo Katoliki Monze, Zambia na kuhudhuriwa
na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Monze.
Askofu
Raymond Mpezele wa Jimbo Katoliki Livingstone katika mahubiri yake wakati wa kumweka
wakfu Askofu Moses Hamungole ameitaka Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Monze, kumpokea
na kumwonesha ushirikiano wa dhati, Askofu Hamungole, pamoja na kuendelea kumsindikiza
katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka yao ya kila siku. Amemtaka
Askofu Hamungole, kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kumwongoza katika hekima
na busara, katika imani na mapendo kwa ajili ya sifa na utukufu wa Kanisa la Kristo.
Askofu raymond Mpezele amemwomba, Askofu Hamungole kuwa na ujasiri pamoja
na kujiaminisha kwa Yesu Kristo ambaye ni Bwana wa mavuno na daima aendelee kumwambia
kwa njia ya maisha na matendo yake, "Bwana kaa nasi" kama walivyofanya wale wanafunzi
wa Emmau, waliokuwa wamesikitishwa sana kutokana na mateso na kifo cha Kristo, kiasi
kwamba, matumaini yao yalianza kuyeyuka kama mshumaa! Lakini walipokutana na Yesu
Mfufuka, akawafafanulia Maandiko Matakatifu na kuumega Mkate pamoja nao, wakamtambua
na hapo wakajawa furaha, nguvu na ari mpya kiasi cha kurudi tena Yerusalemu ili kutangaza
ufufuko wa Kristo.
Naye Askofu mstaafu Emilio Patriarca wa Jimbo Katoliki Monze,
ameishukuru Familia ya Mungu Jimboni humo kwa ushirikiano mkubwa waliomwonesha wakati
wote alipokuwa anawahudumia kama Askofu na kwamba, wanastahili kupendwa na kuheshimiwa.
Askofu
Moses Hamungole amemshukuru Mwenyezi Mungu na Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteuwa
kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Monze, hata bila mastahili yake. Amemwomba Askofu mkuu
Julio Murat, Balozi wa Vatican nchini Malawi na Zambia kumfikishia Baba Mtakatifu
Francisko salam zake za shukrani. Amewashukuru Maaskofu Emilio Patriarca, George Lungu
na Raymond Mpezele waliomweka wakfu na kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Monze.
Askofu
Hamungole amemshukuru kwa namna ya pekee Askofu mkuu Telesphor Mpundu wa Jimbo kuu
la Lusaka, Zambia kwa ushirikiano mkubwa aliomwonesha alipokuwa Padre wa Jimbo la
Lusaka. Anawaomba waamini wa Jimbo Katoliki Monze kushirikiana na kushikamana na kutembea
kwa pamoja ili kujenga Kanisa na kumshuhudia Kristo kwa njia ya imani tendaji. Waamini
wote wanaalikwa na Kristo kushiriki kikamilifu katika kutangaza Injili ya Furaha.
Askofu
Hamungole anasema, anapenda kujiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Roho Mtakatifu
ili aweze kuwasaidia kupambanua mahitaji na vipaumbele kwa ajili ya maisha na utume
wa Kanisa Jimbo Katoliki Monze! Mipango na mikakati itafanywa kwa kuishirikisha mihimili
mikuu ya Uinjilishaji pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati.
Itakumbukwa
kwamba, Askofu Moses Hamungole alizawali miaka 47 iliyopita na baada ya masomo na
majiundo yake ya Kikasisi, akapdrishwa kunako mwaka 1994. Katika maisha yake kama
Padre amewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Televisheni cha Jimbo kuu la Lusaka, Zambia.
Aliwahi kuteuliwa kuwa Katibu wa Idara ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya
Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA na wakati huo huo, alikuwa ni Rais
wa SIGNIS, Afrika. Kabla ya kuteuliwa kwake kuwa Askofu wa Jimbo la Monze, Zambia,
alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Idhaa ya Kiingereza na Kiswahili ya Radio Vatica.
Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican inamtakia kheri na baraka katika maisha na utume wake
mpya kama Askofu wa Jimbo Katoliki Monze, Zambia.
Imeandaliwa na Padre
Richard A. Mjigwa. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.