2014-05-09 07:03:33

Wadau wa elimu kufunika mjini Vatican, Jumamosi jioni!


Zaidi ya wadau wa elimu elfu kumi kutoka sehemu mbali mbali za Italia wanatarajia, siku ya Jumamosi jioni tarehe 10 Mei 2014 kukutana na Baba Francisko, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kushiriki katika tukio lililoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linalohimiza mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu. RealAudioMP3

Kauli mbiu inaonesha kwamba, Kanisa daima limekuwa ni mtetezi na mhudumu mkuu wa sekta yaelimu, kumbe kuna haja kwa serikali kuweka sera na mikakati inyoheshimu usawa katika kuchangia sekta ya elimu badala ya mfumo uliopo kwa sasa unaoonesha ubaguzi kwa shule zinazoendeshwa na kumilikiwa na Kanisa.

Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema kwamba, Kanisa limekuwa ni mdau mkuu katika sekta ya elimu, jambo linalojionesha hata katika historia. Kanisa limesaidia kuwafunda watu huru na wa kweli wanaoweza kusimamia ukweli na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, usawa, umoja, upendo na mshikamano wa kweli.

Kanisa kwa kukutana na kushirikiana na Baba Mtakatifu Francisko linataka kuonesha kwamba, liko imara kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya sekta ya elimu, linataka kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi. Tukio hili linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Hii itakuwa ni mara ya kwanza katika historia nchini Italia, wadau wa sekta ya elimu katika ujumla wao kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu, kwa ajili ya kutetea mafao ya wengi.








All the contents on this site are copyrighted ©.