Mashemasi 13 kupewa Daraja Takatifu la Upadre mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 11 Mei 2014, Siku ya kuombea miito, anatarajiwa
kutoa daraja takatifu la Upadre kwa Mashemasi 13 kutoka Jimbo kuu la Roma. Mashemasi
hawa walipata bahati ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko tarehe
25 Aprili 2014, ili kuwafahamu kabla ya kuwapadrisha.
Monsinyo Guido Marini,
mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa ametoa ratiba elekezi za Ibada mbali mbali zinazotarajiwa
kuadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Mei, 2014, mwezi uliotengwa maalum
kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria.
Baba Mtakatifu Jumapili tarehe 11 Mei
2014, Jumapili ya nne ya Pasaka, Siku ya hamsini na moja ya kuombea miito mitakatifu
ndani ya Kanisa inayoongozwa na kauli mbiu “Miito, ushuhuda wa ukweli” anatarajiwa
kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican
sanjari na kutoa Daraja Takatifu la Upadre. Ibada hii ya Misa Takatifu inatarajiwa
kuanza majira ya saa 3:30 kwa saa za Ulaya.
Jumapili tarehe 18 Mei, 2014, Baba
Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Parokia ya Madhabahu ya Bikira Maria wa
Upendo wa Mungu au kama inavyojulikana kwa wenyeji “Santa Maria del Divino Amore”.
Hija hii ya kichungaji itafanyika majira ya saa 10: 00 Jioni kwa saa za Ulaya.
Ili
wote wawe wamoja ndiyo kauli mbiu inayoongoza Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko
katika Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014, kama sehemu ya Maadhimisho
ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana na kusali pamoja na Patriaki
Anathegoras wa Yerusalemu, tarehe 5 Januari 1964.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican itaendelea kukushirikisha yale yanayojiri katika maisha na utume wa Kanisa.
Kwa wale wenye haraka zao, wanaweza kutembelea kwenye mtandao wa Radio Vatican kwa
habari zaidi.