2014-05-09 09:19:59

Majadiliano ya kiekumene yajikite katika mahangaiko ya Wakristo!


Patriaki mkuu Karekin wa Pili, Mkuu wa waamini Wakatoliki wa Armenia pamoja na ujumbe wake, Alhamisi tarehe 8 Mei 2014 wamekutana, wakasali na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, ili kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, ambaye amependa Makanisa haya mawili kuendelea kushikamana, katika upendo na udugu, kwa kushirikiana ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza duniani.

Patriaki mkuu Karekii wa Pili amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, bado anaendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala. Amemshukuru kwa ushupavu na majitoleo yake ya kichungaji, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa Katoliki sanjari na kuendelea kuimarisha imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi kwa kusimama kidete kulinda na kutetea: utu na heshima ya binadamu, amani na utulivu kati ya watu.

Patriaki mkuu Karekin wa Pili amempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume miongoni mwa vijana, lakini zaidi kwa kuwa ni sauti ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni wa Jamii, mambo ambayo yanaendelea kuwahamasisha watu kulipenda Kanisa la Kristo. Anasema, kwa upande wake, Kanisa nchini Armenia linajielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha uhuru, haki na amani.

Kanisa linaendelea kuwekeza katika majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuhimiza ushirikiano kati ya Makanisa, ili kwa pamoja kuweza kujifunga kibwebwe kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza duniani.

Wakati huu nchi mbali mbali zinapofanya kumbu kumbu ya Vita kuu vya Dunia ambavyo vimepelekea maafa makubwa kwa watu, katika Karne ya ishirini, anasema, kuna haja ya kulaani vita inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia kwani ni chanzo kikuu cha umaskini na mateso na mahangaiko ya watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao ili kuokoa maisha yao. Historia inaonesha kwamba, hata leo hii bado kuna mauaji ya kimbari yanaendelea duniani.

Patriaki Mkuu Karekin wa Pili ametumia fursa hii kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Armenia kunako Mwaka 2015 katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka mia moja ya "dhambi kubwa" ili kusali kwa ajili ya kuwaombea mashahidi hawa wa imani na amani na kwamba, wanatarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu na Kanisa la Armenia. Amemwomba Mwenyezi Mungu awaongoze katika njia ya haki na amani, ili waendelee kutekeleza mapenzi yake, kwa sasa na kwa siku zote, amina!







All the contents on this site are copyrighted ©.