2014-05-09 15:17:38

Kanisa ni Jumuiya ya watu wanaoishi Heri za Mlimani, nyumba ya maskini na wote wanaodhulumiwa!


Waraka wa Injili ya Furaha "Evangelii Gaudii" ni mwaliko kwa waamini kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji ambao ni msingi wa maisha na utume wa Kanisa. Bado kuna haja ya kwenda nje ya mipaka iliyotolewa ushuhuda wa pekee na Wamissionari watakatifu na wakarimu ili kushiriki katika kuimarisha miundo mbinu ya Uinjilishaji ili kuendeleza dhamana ya Umissionari ndani ya Kanisa.

Uinjilishaji katika ulimwengu wa utandawazi unaojikita katika mabadiliko makubwa ya kijamii, unalitaka Kanisa kuwa ni la Kimissionari linalotoka nje ili kuinjilisha, kwa kufanya mang'amuzi ya kina kuhusu tamaduni na mwono wa mwanadamu. Kanisa halina budi kubadilika na kujikita zaidi na zaidi kwa Kristo, ili kutafakari pamoja na kuungana na Kristo pamoja na Roho Mtakatifu, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu analiwezesha Kanisa kuona njia, mbinu na mifumo mipya ya Uinjilishaji.

Roho Mtakatifu analijalia Kanisa nguvu ya kujikita katika hija ya kimissionari ili kutangaza Injili ya Furaha, ili watu wengi zaidi waweze kuangaziwa na mwanga wa Kristo, kwa wale waliosikia Habari Njema na wale ambao wamekataa kumkubali Yesu. Ndiyo maana Mama Kanisa anawahamasisha waamini kutoka kifua mbele ili kuwatangazia wote Habari Njema ya Wokovu, kwani watu wana kiu ya kusikia Injili ya Kristo! Watu wasifungwe na udhaifu na dhambi binafsi mambo yanayoweza kukwamisha ushuhhuda na utangazaji wa Injili. Mchakato wa kukutana na Yesu unawajalia waamini furaha ya kumtangaza Yesu kwa kila kiumbe!

Hii ni hotuba ya iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 9 Mei 2014, kwa Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa waliokuwa wanafanya mkutano wao wa mwaka mjini Roma. Baba Mtakatifu anasema kwamba, Kanisa kwa asili ni la kimissionari na linawajibika kutekeleza huduma ya upendo kwa wote na kwamba, mshikamano na udugu ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake duniani na kwa ajili ya dunia.

Uinjilishaji unawalenga wote, lakini kwanza kabisa hauna budi kuwafikia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, watu wanaelemewa na mzigo wa maisha, ili kuendeleza utume wa Yesu aliyeyamimina maisha yake, ili watu waweze kupata utimilifu wa maisha. Kanisa ni Jumuiya ya watu wanaoishi Heri za Mlimani, nyumba ya maskini na wote wanatengwa na kudhulumiwa; ni kwa ajili ya watu wenye njaa na kiu ya haki.

Ni jukumu la wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kuhakikisha kwamba, Jumuiya za Waamini zinapokea na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini pamoja na kuacha milango yake wazi kwa wale wanataka kupata hifadhi! Mashirika haya ni nyenzo muhimu sana katika utekelezaji wa ukarimu katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu, changamoto na mwaliko wa kutekeleza dhamana hii kwa uvumilivu na uwajibikaji wa kimissionari. Kuna kundi kubwa la Familia ya Mungu linalohitaji kuonja upendo wa Kristo ili kukuza ari na mwamko wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa njia ya Uinjilishaji.

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni, anawashukuru wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kwa majitoleo yao katika huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaopania kuwaonjesha watu wote upendo na mwanga wa Kristo. Bikira Maria awasindikize na kuwasaidia katika dhamana ya Uinjilishaji.







All the contents on this site are copyrighted ©.