2014-05-09 08:14:46

Bara la Ulaya linahitaji kujisimika katika mshikamano, kwa kuheshimu utu wa binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa washiriki wa mkutano mkuu wa sitini na tatu wa Shirikisho la Vyuo vikuu vya Kikatoliki nchini Italia, F.U.C.I, unaoongozwa na kauli mbiu "Bara la Ulaya njia panda: safari ya mwingiliano kuelekea Bara Jipya", anawatakia kheri na baraka wajumbe wote wanaoshiriki katika mkutano huu mjini Padova, Kaskazini mwa Italia.

Mkutano huu umefunguliwa Alhamisi jioni tarehe 8 Mei 2014 na unafungwa rasmi hapo tarehe 11 Mei 2014. Kati ya mada zinazochambuliwa ni: utamaduni na umoja Barani Ulaya; tofauti katika maridhiano, licha ya myumbo wa uchumi kimataifa, Bara la Ulaya limejengeka katika misingi ya utamaduni. Wajumbe wanaendelea kuchambua uhusiano kati ya Bara la Ulaya na: Kanisa, Utamaduni na uchumi.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hizi ni mada zinazoendelea kutoa changamoto kubwa katika medani za kimataifa, kwa kuangalia pia uhusiano uliopo kati ya Jamii na Kanisa pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwashirikisha watu Barani Ulaya; pamoja na kufanya upembuzi wa kina kati ya imani ya Kikristo na Umoja wa Ulaya, kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu zinazojionesha katika mawazo, sanaa na tamaduni Barani Ulaya, ili kujenga na kudumisha mshikamano pamoja na kuheshimu utu wa binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.