Familia ya Mungu huko Jordan inaendelea na maandalizi kamambe kwa ajili ya hija ya
kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei, 2014,
itakayomwezesha Baba Mtakatifu kutembelea: Yordan, Palestina na Israeli.
Katika wimbo
rasmi kwa ajili ya mapokezi ya Baba Mtakatifu, waamini kutoka Jordan wanamwimbia Mwenyezi
Mungu kwamba, ni mwingi wa huruma na mapendo, amlinde na kumwongoza Papa Francisko
anapotembelea Nchi Takatifu, mahali alipozaliwa Yesu, akabatizwa, akafundisha, akateswa,
akafa na kufufuka kutoka katika wafu.
Wanamwomba Mwenyezi Mungu awe pamoja
na Papa Francisko, ambariki na kumlinda kila hatua atakayofanya kati ya ndugu zake
katika imani, ili kwamba, hija yake ya maisha ya kiroho, iwawezeshe watu wengi zaidi
kumwona mwalimu mwenye busara na kiongozi mnyenyekevu. Wanaomba ili hija ya kichungaji
ya baba Mtakatifu iwe kweli ni chemchemi ya haki, amani na utulivu huko Mashariki
ya kati.
Waamini wanasali sala hii kila siku na wakati wote waamini wanapokutana
katika Ibada, Liturujia au mkutano. Huu ni mkazo ambao umetolewa na Askofu mkuu Maroun
Lahham wa Jimbo kuu la Amman, Yordan. Waamini katika mwezi Mei, uliotengwa maalum
kwa ajili yak usali Rozari takatifu, wanamkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko,
ili Bikira Maria aweze kumwongoza katika hija yake ya maisha ya kiroho. Hivi ndivyo
waamini kutoka Yordan wanavyoendelea kujiandaa kiroho kwa ajili ya hija ya kichungaji
itakayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko huko Mashariki.
Katika sala na nia
zao, wanaendelea pia kusali kwa ajili ya kuombea umoja na mshikamano miongoni mwa
Wakristo, kama kielelezo cha kukoleza ushuhuda wa pamoja katika mchakato wa Uinjilishaji
mpya. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Costantinopoli atakutana na kusali pamoja
na Baba Mtakatifu Francisko, kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya hija ya kichungaji
iliyofanywa na Papa Paulo VI kwa kukutana na kusali na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu.
Ili wote wawe wamoja ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu
Francisko katika Nchi Takatifu.
Waamini wanaendelea kusali, ili kwamba, mkutano
kati ya Baba Mtakatifu na viongozi mbali mbali wa Serikali na Siasa, uweze kuamsha
tena ari na moyo mpya wa kutaka kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na
utulivu kati ya watu. Wanamwombea Baba Mtakatifu ili aweze kuwaimaarisha ndugu zake
katika imani na kuwakirimia utambulisho wa Kikristo wanaopaswa kuutolea ushuhuda hata
katika mazingira magumu kama ya kwao!
Usuhuda uoneshe Fumbo la Pasaka, yaani
mateso, kifo na ufufuko wa Kristo; matumaini kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa
na makazi ya kudumu, bila kuwasahau maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni wa jamii.