2014-05-07 07:02:51

Yaliyojiri Jimboni Mpanda!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Bernadin Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa kuwa msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki la Dodoma, baada ya Baba Mtakatifu kumhamisha Askofu Gervas Nyaisonga kwenda Jimbo Katoliki la Mpanda na kusimikwa rasmi tarehe 4 Mei 2014 katika Ibada iliyoongozwa na Askofu mkuu Francisco Montercillo Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zilizosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Padilla anamtakia utume mwema unaosimikwa katika utii na unyenyekevu na majitoleo kwa ajili ya Familia ya Mungu Jimboni Mpanda. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumpokea na kushirikiana na Askofu Gervas Nyaisonga kwa mikono miwili, ili aweze kutekeleza utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu. Waamini wamchukulie si tu kama mchungaji mwema, bali kama baba na rafiki katika Parokia na nyumba zao.

Baba Mtakatifu anamtaka Askofu Nyaisonga kujitoa bila ya kujibakiza pamoja na kuendelea kujibidisha kuwatafuta Kondoo, lakini hasa zaidi wale walipotea, ili kuwasaidia tena kurudi nyumbani, ili waonje huruma na upendo wa Mwenyezi Mungu. Kama Askofu aendelee kutoa faraja kwa wale waliokatika shida na magumu ya maisha kwa kuendelea kutekeleza utume ulioanzishwa na Yesu wa kuwahubiria watu Habari Njema ya Wokovu, kwa kupita katika miji na vijiji vya watu.

Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mpanda inapaswa kuguswa na huruma na upendo wa Mungu kutokana na majitoleo yanayooneshwa na Askofu Nyaisonga. Bila shaka ataendelea kuwa ni Msamaria mwema, kwa kuwasikiliza, kuwahudumia na kuwaganga waamini wa Jimbo Katoliki Mpanda: kiroho na kimwili. Amewataka waamini kujiruhusu kufundwa na Yesu kwa kusikiliza Neno la Mungu, maisha ya sala na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi Sakramenti ya Ekaristi takatifu inayopaswa kuadhimishwa kwa uchaji na ibada.

Kwa njia ya maadhimisho haya Mwenyezi Mungu atatukuzwa na mwanadamu kutakatifuzwa; upendo na udugu vitaweza kujengeka na kushamiri kati ya watu na kwamba, kwa njia ya Ekaristi waamini wa Jimbo Katoliki Mpanda wanaweza kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Baba Mtakatifu katika salam zake, amemshukuru Askofu Damian Kyaruzi wa Jimbo Katoliki Sumbawanga kwa kulisimamia Jimbo Katoliki la Mpanda hadi wakati huu linapopata mchungaji mkuu.

Askofu Kyaruzi katika mahubiri yake, amewataka waamini wa Jimbo Katoliki Mpanda kuwa na imani thabiti na kamwe wasikate tamaa. Askofu Nyaisonga atawasindikiza kwa njia ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa pamoja na mashauri yake ya kibaba!

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, amemtaka Askofu Nyaisonga kusindikizwa na mang’amuzi makuu, busara na hekima, ili kuendeleza na kuboresha yale yaliyoanzishwa na mtangulizi wake. Ameitaka Familia ya Mungu kumpatia ushirikiano wa dhati, ili Askofu Nyaisonga aweze kutekeleza wajibu wake barabara katika mchakato wa uinjilishaji.

Mkuu wa mkoa wa Katavi Dr. Rajabu Lutengwa, kwa niaba ya Serikali ameahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa Askofu Nyaisonga katika utekelezaji wad hamana na utume wake Jimboni Mpanda, ili kuendeleza mipango na mikakati ya maendeleo ya watu kiroho na kimwili. Mkoa wa Katavi kuna fursa nyingi za maendeleo, ambazo zikitumika barabara zitakuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wa Mpanda na Katavi katika ujumla wake.

Mama Tunu Pinda, mke wa Waziri mkuu wa Tanzania amelishukuru Kanisa kwa kuwapatia tena mchungaji mkuu baada ya kifo cha Askofu Paschal Kikoti. Amewataka waamini kuendelea kujikita katika sala bila kutoa nafasi kwa Shetani ambaye anaweza kulisambaratisha Kanisa.








All the contents on this site are copyrighted ©.