Mama Kanisa anaendelea kuwekeza katika utume kwa vijana wa kizazi kipya kwa kuwataka
kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, hasa wakati huu Mama Kanisa
anapoendelea kujielekeza katika Uinjilishaji Mpya unaogusa mahitaji ya mtu mzima.
Anawataka
vijana kulifahamu Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Mafundisho Jamii ya Kanisa
pamoja na kujikita katika maisha ya sala, kama njia ya kuzungumza na kujadiliana na
Mwenyezi Mungu.
Vijana wanahimizwa kujenga na kudumisha: Imani, matumaini,
mapendo na urafiki na Kristo kwani, kamwe hatawadanganya wala kuwatelekeza katika
matumaini na mahangaiko yao ya ndani. Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha vijana
kufanya tafakari ya Heri za Mlimani kwani haya ni Mafundisho Makuu ya Yesu aliyoyatoa
pale kando la Ziwa la Galilaya.
Mlimani kadiri ya Maandiko Matakatifu ni mahali
pa ufunuo ambako Mwenyezi Mungu anapenda kukutana na watu wake. Yesu anatumia fursa
hii ili kuwashirikisha wafuasi wake chemchemi ya maisha, kwa kujifunua kama Mwalimu
na Musa mpya.
Hii ndiyo changamoto iliyowakutanisha Vijana Wakatoliki 850 kutoka
katika shule za Sekondari 90 zilizoko Jimbo Katoliki la Moshi, wakati wa maadhimisho
ya Tamasha la Pasaka kwa mwaka 2014. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, wito ni mwaliko
na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo inapokelewa na kumwilishwa katika
hali ya neema, kwa kupenda na kukumbatia wito huo. Ni maneno yaliyotolewa na Padre
Mathew Mushi kutoka Jimbo Katoliki Moshi wakati alipokuwa anazungumza na vijana wakatoliki
kutoka Jimbo Katoliki la Moshi.
Vijana wamekumbushwa kwamba, wito wa ndoa ni
msingi wa miito mingine yote ndani ya Kanisa. Miito ya upadre na maisha ya kitawa
ni maalum kwa ajili ya huduma kwa Familia ya Mungu. Mapadre na watawa wanapaswa kuonesha
mifano bora ya maisha, kama ushuhuda wa nguvu ya upendo wa Mungu na maisha ya sadaka
yanayofumbwa katika hija ya maisha yao ya kila siku, kwa ajili ya sifa na utukufu
wa Mungu na Kanisa lake. Hili ni kundi maalum ambalo linajisadaka kwa ajili ya huduma.
Ni watumishi wa Injili wanaoitwa kushuhudia kwa namna ya pekee mashauri ya Kiinjili
katika maisha na vipaumbele vyao.
Tamasha la Pasaka anasema Padre Valens Assenga,
Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi, Jimbo Katoliki Moshi, huwahusisha vijana wakatoliki
wanaosoma kwenye shule za sekondari na huadhimishwa mara baada ya Siku kuu ya Pasaka
kila mwaka.
Tamasha la mwaka 2014 limegusia pamoja na mambo mengine kuhusu:
hija ya maisha ya imani ya mwanafunzi mkatoliki; changamoto za kiimani, maisha ya
mwanafunzi mkatoliki shuleni; wito wa upadre na utawa; umuhimu wa elimu pamoja na
mahusiano ya mwanafunzi anapokuwa nyumbani, shuleni na katika ulimwengu ambao kwa
sasa ni kamka tambara bovu!
Tamasha hili kwa namna ya pekee, ilikuwa ni fursa
kwa Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kimissionari kujinadi kwa kuwaelezea
vijana wakatoliki karama na utume wao ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake.
Kwa mkurugenzi wa miito Jimbo Katoliki Moshi, ilikuwa ni fursa ya kutoa mwaliko kwa
vijana kukumbatia heri za mlimani kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko ili waweze
kujisadaka kwa ajili ya Mungu, Kristo, Kanisa na Ulimwengu!
Baba Mtakatifu
Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Vijana Kijimbo, iliyoadhimishwa wakati wa
Jumapili ya Matawi amewakumbusha kwamba, Yesu anajionesha kuwa ni njia inayobubujika
furaha tangu pale alipozaliwa hadi alipokufa juu ya Msalaba na hatimaye, kufufuka
siku ya tatu, matukio yote haya yanaonesha jinsi ambavyo alimwilisha Heri za Mlimani
katika maisha yake na kukamilisha ahadi za Ufalme wa Mungu. Yesu anawaalika wafuasi
wake kutembea pamoja na ye katika njia ya upendo inayowapeleka katika uzima wa milele.
Hii ni njia inayosheheni magumu, lakini Yesu ameahidi kwamba, ataendelea kuwa
pamoja nao hadi utimiifu wa dahali. Watakumbana na umaskini, watateswa na kunyanyaswa,
watapamba na na ukosefu wa haki na changamoto za toba ya wongofu wa ndani, bila kusahau
mapambano yanayowataka kuchuchumilia utakatifu wa maisha.
Kwa hakika anasema
Baba Mtakatifu, watakabiliana na changamoto mbali mbali za maisha, mwaliko wa kuendelea
kushirikiana na Yesu katika furaha na mateso, katika magumu na hali ya kukata tamaa.
Kwa kushikamana na Yesu anasema Baba Mtakatifu, waamini wataweza kupata amani na furaha
inayobubujika kutoka kwenye upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Heri za Mlimani ni
nguvu ya mabadiliko mapya inayoleta mageuzi ya furaha ya kweli na wala si kama ile
inayotolewa na vyombo vya upashanaji habari. Inashangaza masikioni mwetu kwamba, Mwenyezi
Mungu amejitwalia ubinadamu, akawa sawa na binadamu, hata kufa Msalabani.
Kwa
mantiki ya ulimwengu huu, wale ambao wanahesabiwa na Yesu kuwa wana heri, ni watu
wanyonge na waliopoteza dira na mwelekeo! Wanatukuzwa wale wanaoonesha mafanikio,
wenye mamlaka, nguvu na wenye kuheshimiwa na watu! Hii ni changamoto kubwa ya imani,
inayowaalika vijana kuchukua Msalaba wao na kuanza safari ya kumfuasa Yesu, kwani
Yeye anayo maneno ya uzima. Vijana wakithubutu kumkubali na kumpokea Yesu katika maisha
yao ya ujana, atawajaza furaha na maana halisi ya maisha!
Baba Mtakatifu anawahamasisha
vijana kuwa ni watu wenye furaha inayosimikwa katika imani na ukweli, mambo yatakayowawezesha
kuwa na mang’amuzi ya kweli katika maisha kwa kukataa njia za mkato ambazo mara nyingi
zinahatarisha maisha yao kwa kuwatumbukiza katika raha, starehe na anasa, mambo ambayo
kamwe hayawezi kuzima kiu ya maisha yao ya ndani. Inasikitisha kumwona kijana akiogelea
katika utupu!
Vijana wanapaswa kuwa imara wakiwa wanaongozwa na Neno la Mungu
katika maisha yao, tayari kushindana na malimwengu, wakiwa na ujasiri unaowaongoza
kutafuta furaha ya kweli pamoja na kuzingatia mambo msingi katika maisha. Kwa njia
hii vijana wataweza kuwajibika na kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri
mkuu.
Baba Mtakatifu anasema, umaskini wa roho unajionesha kwa namna ya pekee
katika Fumbo la Umwilisho, pale Yesu alipojitwalia hali ya binadamu akawa sawa na
binadamu na wala hakuona kwamba, kuwa sawa na Mungu ni jambo la kung’ang’ania sana.
Hapa Mwenyezi Mungu anaamua kuukumbatia umaskini, ili aweze kumtajirisha mwanadamu
kwa umaskini wake. Hili ndilo Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika
Fumbo la Pasaka, kwa kuonesha unyenyekevu na upendo wa hali ya juu kabisa kwa mwanadamu.
Mtakatifu Francisko wa Assisi ni kielelezo na mfano wa kuigwa katika umaskini wa roho,
kwa kuonesha upendo kwa Kristo, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Umaskini
wa roho ni changamoto na mwaliko wa kubadilisha mfumo wa maisha kwa kuwa huru na vitu
na kutokubali kumezwa na malimwengu, utajiri na mali na matokeo yake mambo haya yanawaachia
machungu katika maisha. Vijana wanahamasishwa kujiaminisha mbele ya Mungu anayewapenda
na kamwe hatawasahau, jambo la msingi ni kuwa na ujasiri wa furaha na kiasi.
Vijana
wanaalikwa na Mama Kanisa kwa namna ya pekee kutubu na kuongoka, kwa kukazia upendo
na mshikamano wa kidugu katika mchakato wa kukabiliana na hali ya umaskini unaojionesha
katika: ukosefu wa fursa za ajira, wahamiaji, matumizi haram ya dawa za kulevya na
utumwa mamboleo. Vijana wawe ni kikolezo cha: ujasiri, upendo na matumaini mapya miongoni
mwa vijana wenzao. Kukutana na Maskini ni fursa ya kukutana na Yesu mteseka!