Swiss guards watakiwa kuwa ni mkate safi kwa wale wanaokutana nao!
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 6 Mei 2014, katika
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa
ajili ya Kikosi cha ulinzi cha Kipapa katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 508
wakati Askari 147 kutoka Uswiss walipojisadaka kwa ajili ya kulinda Kanisa na Papa
Clement VII.
Ibada hii imehudhuriwa na Makamanda, wanajeshi na familia zao
pamoja na viongozi kadhaa kutoka mjini Vatican. Wanajeshi wapya 30 wamekula kiapo
cha utii kwa Baba Mtakatifu.
Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amekazia
umuhimu wa kushiriki kikamilifu na kupokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, ili kuzima
kiu na njaa ya maisha ya kiroho, kielelezo cha imani thabiti. Yesu anasema ni mkate
ulioshuka kutoka mbinguni, kumbe, ni mkate wa maisha ya uzima wa milele na alama wazi
ya uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake anayeendelea kuwaangazia wafuasi wake
kwa njia ya Neno la Mungu na maisha ya Kisakramenti.
Kardinali Parolin anasema,
Kanisa linawakumbuka kwa namna ya pekee Askari 147 waliojisadaka kwa ajili ya kulinda
Kanisa na kumtetea Khalifa wa Mtakatifu Petro, ni mwaliko wa kuchota katika hazina
ya imani, tunu msingi za maisha ya kiroho ambazo zimekuwa kweli ni dira na mwongozo
katika historia ya wanajeshi hawa. Jambo la kwanza ni huduma kwa Kanisa na kwa Khalifa
wa Mtakatifu Petro, kielelezo makini cha ushuhuda na ujasiri kwa Kristo na Kanisa
lake.
Huu ni ujasiri ambao wakati mwingine unaweza kuwagharimu maisha, kama
ilivyokuwa kwa Stefano shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumshuhudia
Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Hata katika majaribu kama
haya, hakuna haja ya kukata tamaa, bali kusonga mbele kwa ari na ujasiri mkubwa ili
kumshuhudia Kristo kwa furaha, imani na matumaini thabiti.
Kardinali Pietro
Parolin amewataka Askari wa Kikosi cha Ulinzi cha Kipapa maarufu kama "Swiss guards"
kuwa mkate safi kwa watu wanaokutana nao mjini Vatican, kwa kuonesha ushuhuda wa furaha
ya Kikristo. Amewataka waendelee kuwa imara na thabiti katika imani, matumaini na
mapendo!