Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon, Jumanne, asubuhi tarehe 6 Mei 2014,
amewasili mjini Juba, Sudan ya Kusini kwa ziara ya siku moja ili kujaribu tena kutoa
ushawishi kwa makundi hasimu nchini humo kuanza tena mazungumzo yanayopania kujenga
na kudumisha amani na utulivu Sudan ya Kusini, ambayo kwa sasa imetumbukia katika
vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo tayari imekwisha sababisha maafa makubwa kwa watu
na mali zao!
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na kuzungumza na viongozi
wakuu wa Sudan ya Kusini ametembelea kambi ya wakimbizi wa Sudan ya Kusini ambamo
kuna zaidi ya watu themanini elfu waliokimbilia humo ili kupata hifadhi kutokana na
vita inayoendelea kurindima nchini Sudan ya Kusini.
Wachunguzi wa masuala ya
kisiasa wanasema, vita na machafuko ya kisiasa yanayoendelea Sudan ya Kusini ni matokeo
ya uchu wa mali na madaraka kutokana na utajiri mkubwa wa mafuta unaopatikana Sudan
ya Kusini, ambao badala ya kuwa ni neema umegeuka kuwa taabu na mateso ya wananchi
wa Sudan ya Kusini, kiasi cha kuanzisha vita na kinzani za kikabila, mchezo mchafu
uliopitwa na wakati!
Katibu mkuu katika ziara yake hii amewataka viongozi wakuu
wa Serikali na wapinzani kusitisha vita mara moja, ili kutoa nafasi kwa wakulima kuendelea
na shughuli za uzalishaji kwani hadi sasa kuna jumla ya watu millioni moja wanaokabiliwa
na uhaba mkubwa wa chakula na kwamba, majadiliano ya amani ni njia pekee ya kumaliza
vita na kinzani za kijamii.