2014-05-07 07:00:30

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kukutana na Papa mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 9 Mei 2014 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon atakayekuwa ameandamana na wakuu wa taasisi za kimataifa kwenye Umoja wa Mataifa. Taarifa hii imethibitishwa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 9 Aprili 2013 alikutana na kuzungumza na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini Vatican, ambaye baadaye alikutana na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati huo. Katika mazungumzo hayo, Baba Mtakatifu Francisko alisema alipenda kuendeleza mazungumzo kati ya viongozi wa Kanisa pamoja na viongozi wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa kudumisha misingi ya haki, amani, mafao ya wengi pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu.

Katika mazungumzo yao viongozi hawa wawili waligusia vita iliyokuwa inaendelea nchini Syria na sehemu mbali mbali za dunia, ambako amani na utulivu bado ni ndoto kwa wananchi wengi. Walizungumzia pia biashara haram ya binadamu inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu; hali ya wakimbizi na wahamiaji.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyekuwa anaanza awamu ya pili ya uongozi wake wa miaka mitano, aliofafanua mikakati ya uongozi wake kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta Mwarobaini wa kuzuia na kutibu vita na kinzani za kijamii zinazoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu; kujenga na kuimarisha mshikamano wa kimataifa; kukuza na kudumisha maendeleoendelevu ya kiuchumi katika usawa.

Baba Mtakatifu Francisko, alikumbushia pia mchango wa Mama Kanisa katika maendeleo ya mtu mzima yanayogusa mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili. Kanisa limeendelea kutoa huduma kadiri ya utambulisho na nyenzo zilizopo, kwa ajili ya kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kanisa linapenda kukazia utamaduni wa watu kukutana na kuzungumza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.








All the contents on this site are copyrighted ©.