2014-05-07 14:09:28

Karama ya ushauri!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 7 Mei 2014 ameendelea na Katekesi kuhusu Karama za Roho Mtakatifu kwa kutafakari juu ya Karama ya Ushauri ambayo ni muhimu sana katika kutoa maamuzi mazito, ni zawadi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu inayoangaza moyo wa mwamini kiasi cha kuwa na ufahamu wa kuweza kuzungumza, kutenda na kuamua katika maisha njia bora zaidi ya kufuata kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Karama ya ushauri unamwongoza mwamini kupitia kwa Yesu kwenda kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, Roho Mtakatifu anawaongoza katika hija ya maisha yao ya kila siku, kwa kushirikiana na wengine ili hatimaye, kuweza kufanya maamuzi thabiti kadiri ya mwanga wa imani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa njia ya Karama ya Ushauri mwamini anaweza kukua na kukomaa katika busara, kwa kujifunza kung'oa ubinafsi, ili kuweza kuona yote katika mwanga na jicho la Yesu. Karama ya ushauri kama yalivyo mapaji mengine yote ya maisha ya kiroho, hayana budi kukuzwa na kuendelezwa kwa njia ya sala, ili kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu, ili kutenda kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Karama hizi si kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi; Roho Mtakatifu anawashauri waamini kwa njia ya maisha na mang'amuzi ya ndugu zao katika Kristo, ndani ya Kanisa. Wakati huu waamini wanaposhukuru kwa Karama ya Ushauri, Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote kujitaabisha kusaidiana katika njia ya imani kwa njia ya unyenyekevu wanapoendelea kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu inayozungumza kutoka katika undani wa mioyo yao!

Papa Francisko anawataka waamini wote kuyaweka maisha yao mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa kusikiliza kwa makini, wakati Mwenyezi Mungu anapoongea nao katika sala, ili kuwashauri na kuwaelekeza mambo yepi ya kutenda! Waamini wajifunze kwa dhati kabisa njia bora zaidi ya kuzungumza na kutenda, ili kusaidia mchakato wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha!

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee amewataka waamini kutoka Mashariki ya Kati kuhakikisha kwamba, wanafuata mashauri ya kweli, yanayoongozwa na Roho Mtakatifu, ili wasije wakajikuta wanatumbukia katika utumwa kwa kujikita katika mashauri mepesi mepesi!

Baba Mtakatifu alipokuwa anazungumza na waamini pamoja na mahujaji kutoka Poland anakumbusha kwamba, kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili iliyopita kwenye Kanisa la Mtakatifu Stanslaus kama kielelezo cha shukrani kwa Mama Kanisa kumtangaza Yohane Paulo II kuwa mtakatifu, tayari ameanza mchakato wa hija ya kichungaji nchini Poland, itakayofanyika kunako mwaka 2016 kama kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Papa Francisko anawaalika waamini kufanya hija ya pamoja wakiwa wameshikamana katika upendo na sala pamoja na kuendelea kuiga mfano wa Mtakatifu Yohane Paulo II, daima wakiwa vijana ndani ya Roho Mtakatifu. Amewataka vijana kukataa katu katu kutumia dawa za kulevya katika maisha yao. Anawatia shime wafanyakazi na wafanyabiashara katika kipindi hiki kigumu cha athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Alhamisi tarehe 8 Mei 2014, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anatarajiwa kuongoza Ibada ya Rozari Takatifu, kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, Napoli, Kusini mwa Italia. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana kwa ajili ya kumwomba Bikira Maria ili aweze kulikirimia Kanisa na Ulimwengu mzima: huruma na amani. Anawahimiza waamini kusali Rozari Takatifu, hasa katika Mwezi huu uliotengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya heshima kwa Bikira Maria kwa kusali Rozari.







All the contents on this site are copyrighted ©.