Mfuko wa Centesimus Annus kwa ajili ya Papa kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 10 Mei 2014
utafanya mkutano wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “mafao ya jamii na mwelekeo
wa fursa za ajira: Je, mshikamano na udugu vinaweza kuwa ni sehemu ya maamuzi msingi?”
Hivi karibuni
Baba Mtakatifu Francisko aliwataka wajumbe wa Mfuko huu kutafakari kwa kina na mapana
kuhusu fursa mbali mbali zilizopo katika mchakato wa kukuza na kuimarisha mshikamano
wa kidugu katika mikakati ya kiuchumi. Hivi ndivyo anavyofafanua Bwana Domingo Sugranyes
Bickel, Rais wa Mfuko wa Centesimus Annus, wakati akiwasilisha mada ya mkutano huu
kwa waandishi wa habari mjini Vatican.
Tafakari hii inawajumuisha wasomi, wafanyabiashara
na wawakilishi wa viongozi wa Kanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kuangalia
mwelekeo mpana wa kidunia katika masuala ya kiuchumi na uwezekano wa kutengeneza fursa
za mshikano wa ajira kimataifa.
Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna ongezeko
la watu wenye sifa na utalaam katika kazi na kuna kundi kubwa la watu wasiokuwa na
ujuzi wala utaalam; kundi la kati la wafanyakazi linaendelea kupungua na tofauti kubwa
zinajionesha kati ya wafanyakazi wa viwandani kati ya nchi tajiri duniani na zile
zinazoendelea. Hata katika nchi husika, bado kuna tofauti kubwa kati ya wafanyakazi,
mambo ambayo kwa sasa yanaonekana kuwa kama jambo la kawaida kabisa.
Wajumbe
wa Mfuko huu wanataka kupembua maana ya mshikamano wa kidugu katika masuala ya kiuchumi
na kijamii katika uhalisia wake. Huu ni mchakato unaopania pia kupambana na uhalifu
katika masuala ya uchumi na fedha pamoja na kusaidia mikakati ya misaada ya kijamii.
Wajumbe watapata nafasi ya kuangalia jinsi ambavyo wanaweza kutekeleza dhana ya mshikamano
na udugu katika shughuli zao za uzalishaji na uchumi, mambo yatakayojadiliwa katika
makundi ya wajumbe watakaoshiriki katika mkutano huu na matokeo yake kuchapishwa baada
ya mkutano.
Utu, heshima na maadili ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa
katika shughuli za uzalishaji na uchumi, kwa kuonesha pia moyo wa ukarimu na uwajibikaji,
unaowashirikisha wafanyakazi wengi zaidi. Mafundisho Jamii ya Kanisa ni msaada mkubwa
katika kukuza na kudumisha umoja, udugu na mshikamano katika maeneo ya kazi, changamoto
inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu,
heshima na mafao ya wengi.
Mfuko huu pia kwa mwaka 2014 utafanya semina kuhusu
mageuzi katika mfumo wa fedha na mafao ya wengi; umaskini na uwajibikaji ili kulinda
watu maskini zaidi; ni mambo yatakayojadiliwa huko New York, Marekani na Dublin, Ireland.