2014-05-06 06:59:11

Mji wa Yerusalemu unapaswa kuwa ni kielelezo cha mshikamano, lakini!


Familia ya Mungu Nchi Takatifu imeadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Yesu wakiwa na matumaini ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji kwenye Nchi Takatifu na kwamba, toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi yanayoweza kuwasaidia watu kuvunjilia mbali kuta za utengano ambazo bado zinaugawa mji wa Yerusalem. RealAudioMP3

Patriaki Fouad Twal wa Yerusalem anasema, waamini wameshiriki kwa kiasi kikubwa katika maadhimisho ya Juma kuu, changamoto ya kuendelea kuwa kweli ni chumvi na mwanga wa dunia, kwa njia ya ushuhuda a maisha yao adili na matakatifu, kwa kutambua kwamba, wao wamebahatika kuishi katika maeneo matakatifu, kumbe, wanapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa.

Ufufuko wa Yesu Kristo ni kielelezo cha ushindi dhidi ya nguvu za giza, mauti na kifo, kwa bahati mbaya anasema Patriaki Twal kuna wananchi ambao bado wanaishi katika giza, watu ambao wamebaki Ijumaa kuu katika maisha yao kutokana na vita inayoendelea kurindima huko Mashariki ya Kati na hivyo kupelekea idadi kubwa ya watu kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao.

Bado hata Wakristo wamegawanyika, hali ambayo inaonesha kwamba, kuna haja ya kuendelea kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuponya madonda ya utengano kati ya Wakristo, ili wite waweze kuwa wamoja, kama ambavyo Kristo anasali katika Sala yake ya kikuhani.

Mji wa Yerusalemu unapaswa kuwa ni mji mkuu wa binadamu wote, kwani hapa kuna watu wa kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Ikiwa kama tunu msingi za maisha ya Kiinjili zitatawala na kuongoza maisha ya Familia hii ya Mungu kwa kujikita katika: kupokeana na kusaidiana; kusamehe na kupendana kwa kukumbatia haki, ukweli na mafao ya wengi.

Yerusalemu unapaswa kuwa ni Mji ambao unapokea waamini kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali, lakini kwa bahati mbaya, ni mji ambao umegawanyika na raia wake hawaelewani wala kufahamiana, pengine ndiyo maana hata Yesu mwenyewe aliulilia mji huu, kwani ulikuwa umegawanyika na kusambaratika.

Patriaki Twal anasema, inawezekana kabisa kubomoa kuta za mawe zinazowatenganisha watu, lakini si jambo rahisi kubomoa kuta za chuki, uhasama, woga na hali ya kulipizana kisasi inayojikita katika undani wa mioyo ya watu, ndiyo maana kuna haja ya kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kuanza kutembea katika njia na mwanga mpya wa Kristo Mfufuka, kwa kujikita zaidi na zaidi katika umoja na mshikamano wa kitaifa na maisha ya kiroho.

Ni matumaini ya Familia ya Mungu Nchi Takatifu kwamba, mchakato wa majadiliano ya kiekumene uliodumu kwa takribani miaka hamsini utapata sura na mwelekeo mpya wakati wa hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni hija ya kichungaji inayogusa medani mbali mbali za maisha ya watu.








All the contents on this site are copyrighted ©.