2014-05-06 09:56:06

Kikosi cha ulinzi cha kipapa kinatimiza miaka 508 tangu kianzishwe!


Askofu mkuu Angelo Becciu, katibu mkuu msaidizi wa Vatican amewashukuru Makamanda na Wanajeshi wa Kikosi cha Ulinzi cha Kipapa, maarufu kama "Swiss guards", wakati wa kusherehekea siku kuu yao inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Mei kama kumbu kumbu endelevu ya sadaka ya hali ya juu kabisa iliyotolewa na wanajeshi 147 waliojisadaka kunako mwaka 1527 kwa ajili ya kulinda Kanisa na Baba Mtakatifu Clement VII.

Hii ni siku ambayo pia Wanajeshi wapya wamekula kiapo cha utii kwa kwa Baba Mtakatifu na kwamba, imekwisha gota miaka 508 tangu Kikosi cha Ulinzi cha Kipapa kilipoanzishwa na kwamba kila mwaka kuna vijana kutoka Uswiss wanaofika mjini Vatican kwa ajili ya kutoa huduma ya ulinzi na usalama kwa ajili ya Baba Mtakatifu na Kanisa katika ujumla wake. Askofu mkuu Becciu amewashukuru wote kwa sadaka na majitoleo yao!

Wanajeshi wanahimizwa kusali na kuwaomba watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II waliotangazwa hivi karibuni na Mama Kanisa, ili waweze kuwasaidia katika kutekeleza dhamana na majukumu yao kikamilifu, kwani hawa ni watakatifu ambao walikuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Wanajeshi walioanza rasmi utume wao, wamewekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria.

Baadhi ya Makamanda na wanajeshi wamepewa nishani ya heshima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kutokana na huduma yao iliyotukuka mjini Vatican. Wamekumbushwa kwamba, msingi wa siku kuu hii ni imani na upendo kwa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na moyo wa kifamilia unaowaunganisha wote.







All the contents on this site are copyrighted ©.