2014-05-05 08:07:27

Uvivu ni kichaka cha majanga ya mwanadamu!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Karibu katika kipindi chetu, tukumbushane na kutafakari juu ya thamani ya Kazi. RealAudioMP3

Tunafanya hivyo katika mwezi huu wa tano ambao tuliuanza kwa kumuenzi Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, ambaye Mama Kanisa alipenda kumweka kuwa ni msimamizi na mwombezi wa wote wafanyao kazi zenye kumtukuza Mungu na kuchangia hali njema ya wanadamu.

Tangu mwanzo wa uumbaji, Mungu mwenyewe ametuonesha sisi sote thamani ya kufanya kazi. Ni kwa njia ya Kazi Mungu aliuumba ulimwengu. Na alitupatia sisi wanadamu agizo na wito wa kufanya kazi ili kuutiisha ulimwengu (Mw. 1:28). Nyakati mbalimbali katika historia manabii wa Bwana waliitwa na kushiriki kazi ya Mungu ya ukombozi wa Mwanadamu. Kristo Bwana naye alikuja ulimwenguni humu, akafanya kazi ya kumkomboa Mwanadamu. Mungu katika utatu, amejidhihirisha kuwa ni Mungu wa Kazi. Nasi kwa moyo wa utii kwa Mungu wetu, tunataka kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uadilifu, uli tuutiishe ulimwengu, jujipatie riziki yetu ya kila siku na pia tupate riziki ya kuwasaidia walio wahitaji, wasio na uwezo wa kufanya kazi.

Tafanusi ya kazi nyakati zote inatuambia kwamba, kazi ni shughuli yoyote halali yenye kumpatia mwanadamu riziki. Kwetu sisi tunaomwamnini Mungu, kazi ni utii kwa Mungu, kazi ni shukurani kwa Mungu kwa kuumbwa kwetu kama wanadamu, kazi ni kuendelea kujiumba katika utu. Kufanya kazi ni kushiriki kazi ya uumbaji ya Mungu kwa neno lile ‘...mkaijaze nchi na kuitiisha’.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, kwa njia ya kazi mwanadamu anashiriki kazi ya uumbaji ya Mungu, anaingia katika umoja na Kristo Mtenda kazi na anashiriki katika fumbo la wokovu la Pasaka. Na hiyo ndiyo teolojia ya kazi kadiri ya imani yetu.

Hapo tunaona jinsi kazi inavyotuunganisha na ulimwengu wetu lakini pia na ulimwengu wa kiroho. Kinachotupatia heshima mbele za watu ni aina ya kazi tunayofanya, namna tunavyoifanya na namma pia tunavyotumia mapato ya kazi zetu. Hapa tunapata picha ya wazi kwamba, kazi imeunganika kwa karibu zaidi na utu wa mtu, ndiyo maana wenye busara walisema, kazi ni kipimo cha utu.

Wazee wetu wa Mtaguso wa II wa Vaticani, wakitafakari juu ya wito na thamani ya kazi wanatufundisha juu ya malengo ya utendaji kazi. Lengo la kwanza la kazi ni utawala na ukamilishaji wa ulimwengu. Lengo la pili ni utoaji huduma kwa wengine. Lengo la tatu ni ukuaji binafsi na lengo la nne ni kumpa Mungu utukufu (Taz. Hati Furaha na Matumaini, na 67).

Tunapotafakari juu ya wito na maisha ya Mt. Yosefu kama baba mlishi wa Yesu na Baba mwajibikaji wa familia takatifu ya Nazareti, aliyeitunza familia yake kwa kufanya kazi, na zaidi ya hilo, alimfundisha Mtoto Yesu kufanya kazi, tunataka nasi, familia zetu ZIWE SHULE ZA KAZI. Watoto wafunzwe thamani ya kazi, wafunzwe kupenda kufanya kazi ili kujipatia kipato halali kwa maisha yao.

Endapo watoto wetu hawafundishwi thamani ya kazi katika familia, hapo ndipo kinapozuka kizazi cha watu wanaoona kuwa kazi ni adhabu. Kinazuka kizazi chenye kuendekeza utamaduni wa uvivu., watu ambao hawajiandai kuwa watenda kazi makini katika jamii. Watu ambao pengine hupenda kufanya kazi kidogo na kuvuna mapato makubwa mno, kwa njia zisizo za kiadilifu, hata kwa njia ya kudhalilisha utu wao. Kadiri ya Mtume Paulo, wavivu, wasio penda kazi anawaona kuwa ni watu ‘wahovyo’, kwa sababu wanakuwa ni mizigo inayowaelemea wengine. Na anasema wazi, asiyefanya kazi asile (Rej. 2Thes. 3:10). Mtu asipokula manake atakufa, kwa hiyo mvivu hastahili kuishi.

Utamaduni wa kuchukia kazi, utamaduni wa uvivu ni hatari kubwa sana kwa kanisa na taifa. Ndiyo maana tunazigeukia familia na wote wenye dhamana ya malezi, tuwafundishe watoto wetu kazi. Ile aina ya wazazi na walezi wenye tabia ya kufuga watoto katika uvivu, watambue kuwa ni hatari, wanawaangamiza watoto wao. Kwa nje wanaonekana kama wanawaonea huruma watoto wao wasihangaike na kazi, kwa sababu pesa ipo watenda kazi wapo, hivyo watoto wakae tu, wastarehe. Mwisho wa huruma kama hizo, ni uangamizi.

Familia ya watu wavivu ni kichaka cha matatizo mengi, ni chimbuko la ombaomba, chanzo cha mafarakano mengi na ni hatari kwa amani ya majirani. Uvivu ni moja ya vyanzo vikubwa vya dhambi na kila aina ya uovu na ndiyo maana wachaji wa zamani walisema ‘uvivu ni adui wa roho’. Sisi tunakaza kusema, kazi ni afya na uvivu ni chanzo cha magonjwa ya kimwili, kiakili na kiroho. Kazi ni heshima kwa Mungu, uvivu ni fahari ya shetani na unatufanya tuajiriwe naye. Tukifikiri vizuri tutagundua kuwa dhambi nyingi za mawazo, maneno au matendo huwa tunatenda tunapokuwa wavivu. Uvivu ni mlango wa dhambi nyingi na matatizo mengi.

Taasisi zinazohusika na malezi-elimu kwa vijana wanaokuwa mashuleni, nao waone namna sahihi ya kupandikiza roho ya kupenda kufanya kazi kwa vijana hao wawapo shuleni na baada ya kuwa wamehitimu masomo yao. Ajabu sana nyakati zetu hizi, watu watahitimu masomo na pengine watajaliwa kupata ajira, lakini hawapendi kujituma kufanya kazi walioitafuta, badala yake wataendekeza uvivu tu na kudai mishahara mikubwa na marupurupu mengi.

Matokeo yake hakuna maendeleo yanayoonekana hata kama takwimu zitaonesha kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi. Katika taasisi nyingi za huduma ndani na nje ya Kanisa, kuna vilio vya kukosa huduma stahiki. Sio kwamba wahudumu hawapo. Wapo ila ni wavivu mno. Walipenda ajira tu, hawakupenda kazi. Wanaona kazi ni mzigo, ni bugudha. Hivi hata anayekuja kutafuta kuhudumiwa naye anonekana kuwa ni bugudha. Utamaduni w-hatarishi wa uvivu unaendelea kujengeka na kukomaa katika jamii zetu. Hiyo ni hatari kwa familia ya mwanadamu.

Tukitaka kujenga heshima ya kweli ya jamii zetu, kila mmoja wetu ni vema ajenge dhamiri ya kupenda na kuthamini kazi. Sio tu kutafuta ajira na kuwinda mishahara pasipo kujituma kufanya kazi. Kutokana na dhana hii ya uvivu, itashangaza sana nyakati zetu wote ‘wenye ajira na wasio na ajira’ wanakuwa wavivu na mwishoni mwa siku watalalamika maisha ni magumu. Hata aliyeelimika katika ufundi na kilimo, naye atalalamika sawa na yule ambaye hakubahatika kabisa kwenda shule. Tunadhani wakati umefika sasa, tunahitaji mapinduzi ya kifikra. Dhana ya kazi, uwajibikani na maisha mema vipandikizwe kwa bidii katika kuanzia katika kizazi kichanga.

Pamoja na mwito huo wa kufanya kazi, tukumbuke kwamba katika nyakati zetu hizi kuna watu ambao ni walevi wa kazi. Ni wale ambao kwao kazi ndiyo kila kitu. Wakipata kazi, hawamjali Mungu, wala familia, wala jirani. Wao ni kazi masaa yote, na mwisho wa siku kazi inakuwa ndiyo mungu wao. Tunataka kazi tufanyazo ziendelee kujenga utu wetu na sio kutunyang’anya utu wetu. Kazi isitutenge na Mungu na jirani bali ituunganishe zaidi na Mungu na jirani. Mtakatifu Yohane Paulo II alitufundisha akisema ‘kazi ni sehemu mojawapo inayomsaidia mwanadamu kupata utakatifu’. Endapo tutaiabudu kazi, basi hapo haitatupatia utakatifu bali itatunyang’nya utakatifu.

Tunaomba na kusihi, kwa maombezi ya Mtakatifu Yosefu na kwa heshima kwa Mungu wetu, sote tupende kufanya kazi kiadilifu. Tuimarishwe na Neno lisemalo ‘Mungu hakosi haki, yeye hataisahau kazi mliyoifanya au upendo mliyoonesha kwa ajili yake katika huduma mliyowapa na mnayowapa sasa watu wake....Msiwe wavivu, bali muwe kama wale wanao amini na wenye uvumilivu wakapokea yale aliyoyaahidi Mungu (rej. Ebr. 6:10-12). Kutoka Radio Vatican ni Mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.