Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu ni nyenzo msingi katika hija ya maisha ya kiroho!
Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili
ya tatu ya Kipindi cha Pasaka, tarehe 4 Mei 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican anasema kwamba, hija ya wanafunzi wa Emmau waliotikiswa katika
maisha yao, walionekana kukata tamaa, wakarudi Emmau wakiwa wamesonokena, lakini njiani
wakakutana na Yesu ambaye hawakumtambua.
Yesu akawafafanulia kuhusu Maandiko
Matakatifu juu ya mateso, kifo na ufufuko wa Masiha kama ilivyokuwa imetabiriwa na
Manabii. Baada ya kusikia Neno la Mungu, mioyo ya wanafunzi hawa ikawaka moto wa matumaini
mapya. Wakamkaribisha nyumbani mwao na kumtambua wakati alipokuwa anaumega Mkate,
mara akatoweka machoni pao, wakabaki na mshangao mkubwa!
Hii ikawa ni alama
iliyomtambulisha Yesu Mfufuka miongoni mwa wanafunzi wake, ambao walirejea tena mjini
Yerusalem kuwashirikisha wengine mang'amuzi yao kwamba, walikuwa wamekutana na Yesu
Mfufuka katika kuumega Mkate.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, njia ya Emmau
ni kielelezo cha hija ya maisha ya kiimani: Maandiko Matakatifu na Ekaristi Takatifu
ni mambo makuu yanayomwezesha mwamini kukutana na Kristo. Hata leo hii kuna waamini
wanaokwenda Kanisa wakiwa na wasi wasi, hofu na mashaka mioyoni mwao. Ni watu wanaobeba
matatizo na hali ya kukata tamaa, kiasi hata cha kusahau mpango wa Mungu katika maisha
na hatimaye, kumgeuzia Mungu kisogo.
Neno la Mungu linamwezesha Yesu kufafanua
tena Maandiko Matakatifu ili kuwawashia wafuasi wake moto wa imani na matumaini na
kwa kushiriki Ekaristi Takatifu anawakirimia nguvu. Kwa njia hii, waamini wanaweza
kurudi tena nyumbani wakiwa na furaha kama ilivyotokea kwa wanafunzi wa Emmau. Neno
la Mungu na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya furaha, matumaini
na ari mpya. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kutafakari Neno la Mungu katika hali
mbali mbali za maisha na hapo wataonja uwepo na faraja ya Mungu.
Baba Mtakatifu
anawaalika waamini kumkimbilia Bikira Maria, ili aweze kuwaombea kwa Mwanaye mpendwa,
waweze kuishi mang'amuzi ya wanafunzi wa Emmau, hususan katika maadhimisho ya Ibada
ya Misa Takatifu, ili kutambua neema ya kukutana na Yesu anayewakirimia mabadiliko
ya ndani. Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu ni nyenzo msingi katika hija ya maisha
ya kiroho.