Dr. Olav Tveit Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni amehitimisha hija yake
ya kichungaji nchini DRC ambako alipata nafasi ya kuweza kujionea mwenyewe shida na
mahangaiko; imani na matumaini ya wananchi wa DRC wanaoendelea kupambana na vita pamoja
na kinzani za kijamii. Dr. Tveit amewashirikisha
waamini na watu wote wenye mapenzi mema tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa ufufuko
wa Yesu Kristo hasa nchini DRC, nchi ambayo imesahaulika na matatizo yake yote kufutika
vichwani mwa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa. Mahangaiko na mateso ya wananchi
wa DRC kwa sasa si habari yenye mashiko kwani eti ni “majanga” yaliyozoeleka. Lakini
ikumbukwe kwamba, hakuna jamii inayoweza kuzoea mateso na mahangaiko yanayosababishwa
na vita pamoja na kinzani za kijamii. Kuanzia tarehe 25 Aprili hadi tarehe 2 Mei
2014, Dr. Tveit na ujumbe wake, wakiwa nchini DRC wamekutana na kuzungumza na waamini
pamoja na viongozi mbali mbali wa Makanisa. Mada zilizotawala wakati wa hija hii ya
kichungaji ni: haki na amani; usalama na utulivu nchini DRC na Afrika katika ujumla
wake mintarafu ufufuko wa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Dr. Tveit amewakumbusha
wananchi wa DRC kwamba, ufufuko wa Yesu haukutokea wakati mambo yalipokuwa shwari!
Amefufuka kutoka wafu, ili aweze kukutana na kuwaimarisha wale waliokata tamaa, wanaoendelea
kukumbana na dhuluma na nyanyaso mbali mbali pamoja na ukosefu wa haki msingi za binadamu.
Ufufuko wa Kristo ni kielelezo cha mwanga mpya unaowaangazia wale wanaotembea katika
uvuli wa dhambi na mauti, ili kuona mwanga na kuanza kutembea kadiri ya mpango wa
Mungu katika maisha yao. Ujumbe wa imani na matumaini ni muhimu sana kwa wananchi
wa DRC ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiteseka kutokana na vita isiyokuwa na ukomo
nchini humo; vita ambayo imejikita kutokana na utajiri wa rasilimali zilizoko nchini
humo, utajiri ambao ungeweza kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi
wa DRC, lakini kwa sasa umekuwa ni chanzo cha mateso na mahangaiko yao: kiroho na
kimwili. Dr. Tveit anawahakikishia kwamba, hata wao Yesu Kristo ameteswa, akafa
na kufufuka kwa ajili yao, ili waweze kukombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na
mauti na kwamba, licha ya mateso na mahangaiko yao, iko siku wataona mwanga wa ukombozi
ukiwaangazia, hapo ndipo watakapoanza hija ya haki na amani, upendo na mshikamano. Dr.
Olav Tveit na ujumbe wake, walipokuwa nchini DRC wamekutana na kuzungumza na viongozi
mbali mbali wa Makanisa pamoja na wanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Wamesali
na kushirikishana imani na matumani katika mahangaiko ya wananchi wa DRC.