2014-05-05 08:42:48

Mikakati ya mageuzi ya kiuchumi mjini Vatican


Baraza la Kipapa la uchumi lililoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 24 Februari 2014 hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa kwanza, uliosimamiwa na Kardinali Reinhard Marx, Mratibu wa Baraza la Kipapa la uchumi na kuhudhuriwa na wajumbe kumi na mmoja. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Kardinali George Pell, Rais wa Sekretarieti ya Uchumi pamoja na Monsinyo Brian Ferme, katibu mkuu wa Sekretarieti ya uchumi wamehudhuria pia.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa wajumbe wa mkutano huu aliwakumbusha umuhimu wa Kanisa kutumia rasilimali zake kwa umakini mkubwa kwa ajili ya kusaidia mchakato wa Uinjilishaji pamoja na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Anasema kwamba, mageuzi ndani ya Sekretarieti ya Vatican si rahisi yanahitaji watu kuwa na mwelekeo mpya na kwamba, wajumbe wote wa Baraza hili wana haki sawa.

Mkutano wa Baraza la Kipapa la uchumi umefanyika katika mazingira ya utulivu na mafanikio makubwa kwa kuandika muswada wa katiba ya Baraza, utakaojadiliwa tena wakati wa mkutano ujao utakaofanyika tarehe 5 Julai 2014, ili uweze kuwasilishwa na hatimaye kupitishwa na Baba Mtakatifu. Wajumbe wamesikiliza taarifa ya uchumi na uongozi ya Vatican, COSEA, iliyoundwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 18 Julai 2013. Baraza la Kipapa la uchumi linatarajia katika kipindi cha mwaka huu kufanya mikutano mingine miwili, yaani katika Mwezi Septemba na Desemba.








All the contents on this site are copyrighted ©.