2014-05-05 08:28:52

Kitabu elekezi katika mchakato wa waamini walei kuyatakatifuza malimwengu!


Kardinali Francis Arinze, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Ibada, nidhamu na Sakramenti za Kanisa ameandika kitabu chenye maelezo elekezi kwa waamini walei katika maisha yao ndani ya Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla na kuchapishwa na Kitengo cha uchapishaji cha Vatican, LEV. RealAudioMP3

Katika kitabu hiki, Kardinali Arinze anatambua na kukiri mchango mkubwa unaotolewa na waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na kuyatakatifuza malimwengu, kwani wao ni asilimia 99,9% ya Familia yote ya Mungu. Waamini walei wanapaswa kutambua wito na utume wao ndani ya Kanisa kama wabatizwa, asili ya utume wa waamini walei inayopata chimbuko lake latika Sakramenti ya Ubatizo, inayowachangamotisha waamini walei kushiriki kikamilifu katika ufalme, unabii na ukuhani wa Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha amini na adili.

Watambue tofauti ya kina iliyopo kati ya waamini walei, Makleri na watawa, ili kwa pamoja waweze kushikamana na kushirikiana kwa ajili ya ujenzi wa ufalme wa Mungu duniani. Kardinali Arinze anachota mafundisho yake kutoka katika Nyaraka za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na mchango wa Mtakatifu Yohane Paulo II kuhusu waamini walei pamoja na utajiri mkubwa ulioachwa na Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba na nyaraka zake mbali mbali za kitume.

Kardinali Arinze anawataka waamini walei kutambua mchango na dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa hasa zaidi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha yao.

Waamini walei wanaalikwa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na kujikita katika kuyainjilisha na kuyatakatifuza malimwengu, kwa kushiriki kuunda sera makini zinazojikita katika utu na heshima ya binadamu, mafao na ustawi wa wengi. Waamini walei wanapaswa kutolea ushuhuda makini wa Injili ya Kristo na Kanisa lake, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa maneno na mtendo yao, ili hatimaye, dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Ili Waamini walei waweze kutekeleza dhamana na utume wao wa kuyatakatifuza malimwengu kuna haja ya kuhakikisha kwamba, wanapata majiundo makini na endelevu katika Biblia, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na nyaraka mbali mbali zinazotolewa na Mama Kanisa. Waamini walei wasimame kidete kutoa mwelekeo na dira sahihi ya mafundisho ya Kanisa kuhusu: ndoa na familia; Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; umuhimu wa uhuru wa kuabudu na elimu ya dini shuleni.

Kardinali Francis Arinze katika kitabu chake hiki kipya anaonesha mafanikio yaliyopatikana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa kushirikiana na waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Ni kosa kubwa kuyaangalia maisha na utume wa Kanisa kati ya watu kwa njia ya mfano wa Makleri na Watawa tu kana kwamba, Waamini walei ni watazamaji na wala hawaguswi na maisha na utume wa Kanisa ulimwenguni.

Kardinali Arinze anasema, ndani ya Kanisa kuna kazi na utume unaofanywa na watu tofauti na lengo ni kukamilishana katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Waamini walei wana dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao na katika maeneo mbali mbali kweli za Kiinjili, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.