Kikosi cha ulinzi cha Kipapa ni kielelezo cha sadaka, ukakamavu na ulinzi!
Tarehe 6 Mei 1527 walinzi kutoka Uswiss walijisadaka kwa ajili ya kulinda Kanisa na
Baba Mtakatifu, kielelezo cha ujasiri wa hali ya juu kabisa na uaminifu. Ni mwaliko
kwa Kikosi cha Ulinzi kutoka Uswiss kuendelea kutumikia kwa furaha, licha ya mabadiliko
ya nyakati.
Huduma ya Kikosi hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kweli unaojidhihirisha
kwa sadaka kubwa, muhimu na inayowajibisha. Ni maamuzi ambayo yanasindikizwa kwa namna
ya pekee na familia na jumuiya ambayo imejitaabisha kuwafunda, wote hawa wanapaswa
kushukuriwa!
Hizi ni shukrani za Baba Mtakatifu Francisko kwa Kikosi cha Ulinzi
cha Kipapa wakati huu wanapofanya kumbu kumbu ya sadaka iliyotolewa na wenzi wao kunako
mwaka 1527. Anasema, mji wa Roma una utajiri mkubwa wa mambo ya kale, historia na
utamaduni. Ni mahali ambapo kuna umati mkubwa wa mahujaji na watallii wanaoingia na
kutoka mjini Roma kwa sababu mbali mbali. Hii ni hija ya historia ya watu na wanajeshi
wa Kikosi cha ulinzi cha Kipapa wanashiriki pia.
Kama Kikosi cha Ulinzi cha
Kipapa wanayo dhamana ya kushuhudia utulivu na furaha kwa wale wote wanaofika mjini
Vatican ili kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro au kwa ajili ya kukutana na kuzungumza
na Khalifa wa Mtakatifu Petro, changamoto na mwaliko wa kuwa imara na thabiti katika
imani, wakarimu nao wenye upendo wa dhati kwa wote wanaokutana nao!
Baba Mtakatifu
anakumbusha kwamba, Mwaka 2014 magwanda wanayovaa Askari wa Kikosi cha ulinzi cha
Kipapa yanatimiza miaka mia moja, kielelezo cha majitoleo, ukakamavu na ulinzi. Ni
magwanda yanayoonesha utukufu wa historia iliyopita, lakini ndani ya maganda haya
kuna mtu mzima; kuna familia na mahali anakotoka mtu, matumaini na mipango ya maisha.
Ni magwanda yanayodai uungwana, ukarimu na upendo.
Baba Mtakatifu anasema,
hii ni changamoto pia kwa Askari wa Kikosi cha ulinzi cha Kipapa kujenga na kudumisha
maisha ya kijumuiya, wakati wa raha na karaha, kwa kufarijiana na kusaidiana katika
urafiki bila kushabikia mambo yanayoweza kuwagawa na kujikuta wanaelemewa na hali
ya kutojali, nyanyaso na ubaguzi wa rangi.
Baba Mtakatifu anasema, kila siku
yuko karibu na majitoleo na sadaka yao, jambo ambalo anapenda kuwashukuru kwa dhati
kabisa. Anaendelea kuwahimiza kuwa waaminifu kwa kutambua kwamba, Kristo daima yuko
karibu nao anawaunga mkono katika safari yao, hasa wakati wanapochoka na kuwa na wasi
wasi. Baba Mtakatifu amewaweka Wanajeshi wa Kikosi cha ulinzi cha Kipapa chini ya
usimamizi wa Bikira Maria pamoja na watakatifu somo na wasimamizi wao: Nikolaus, Sebastian
na Martini.