2014-05-03 16:25:13

Yaani, imekula kwao!


Kuna msemo ulioshamiri sana kwa Waswahili, hasa ikiwa mtu anayo matumaini ya kupata kitu katika biashara na anakikosa anaambiwa: “Imekula kwako”. Usemi huu ungeweza pia kutumika kwa mitume baada ya kifo na kuzikwa kwa Yesu. Mitume na wafuasi waliweka matumaini yao yote kwa Yesu, lakini sasa baada ya kufa kwake na kupita siku mbili tatu, wanakata tamaa na kujisikia “imekula kwao.”

Wengi wao waliingiwa na woga na kujifungia kwenye vyumbani, ili mradi tu kwamba walikuwa wameishiana na mradi wa kumfuata Yesu. Wengine baada ya kwisha tu sikukuu ya Pasaka ya kiyahudi siku iliyofuata kila mmoja akaanza kuchukua njia zake. Wafuasi wawili walitanguzana mmoja hatajwi jina na mwingine anaitwa Kleopa wakachukua zao kurudi kijijini Emmaus. Wamepoteza muda mrefu wa kutumaini, wa kujitoa, myaka mitatu ya ushindi mkuu, miaka ya imani, ya kusubiri, ya uzuri, miaka utamu ya mwanga. Lakini kifo kile cha Yesu ndicho kilichochafua kila kitu. Ama kweli imekula kwao!

Wafuasi hawa wawili walijisikia kuwa kama miali ya moto inayokaribia kuzimika. Hebu tuone jinsi Bwana mfufuka anavyoihuisha tena: Wafuasi hao wanatembea kwenye barabara kuu wanayopita watu wote, wakiwa katika huzuni kubwa, katika upweke, wakijadiliana. Yesu hawaiti toka mbali na kuwasimamisha, bali anawasogelea kama mtu mwenye haraka lakini anayetaka kutanguzana nao. Wao wanageuka na kugundua kwamba kuna mtu anawafuata. Hapa Yesu amejionesha kama msafiri wa kawaida tu ila mwenye haraka. Yeye mfufuka angeweza kusafiri kwa mwendo wa kasi sana, kumbe anatanguzana nao, anapima hatua zao zilingane na mwendo wao wa kuchoka, mwendo wa waliojeruhiwa.

Wanaelekea Emmaus, yaani anatanguzana nao katika kuchanganyikiwa kwao na katika matatizo na uchungu wao. Ndivyo Yesu anavyokutana na watu mbalimbali hapa duniani na kutanguzana nao katika safari yao ya maisha. Kila mmoja anamkuta akiwa na hali fulani ya pekee.

Tunasikia kwamba Magdalena alimkuta akiwa analia, kwa wale kumi na mmoja kule kwenye ziwa jumapili ijayo, anawakuta wana uchungu na wamechanganyikiwa baada ya kukesha usiku mzima wakivua bila kupata kitu, wakati Tomaso jumapili iliyopita alimkuta katika hali ya kutoamini. Wafuasi hawa anawakuta katika lindi la uchungu na la upweke. Wako wawili tu, lakini sasa wanakuwa wasafiri watatu.

Katika uchungu wao huo wanajadiliana na kuhubiriana juu ya suala zito na muhimu la maisha. Wanaongeana juu ya jambo linalowakereketa kabisa ndani ya mioyo yao. Wafuasi hawa wanazungumza juu ya Upendo. Yaonekana amewakimbilia, na kuwakuta ili kuwapa moyo, kuwahimiza na kuwangaza. Hawakatishi mazungumzo yao: Anatafuta mwanya wa kujiingiza katika mazungumzo yao kwa utulivu, kwa utamu kwa kuuliza swali jepesi na rahisi tu.

Tena anauliza kama vile mtu mjinga asiyefahamu kilichotokea. “Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea?” Kwa swali hili Yesu anaonesha kuujali sana uchungu wao.

Swali hilo linamfanya Kleopa na mwenzake waanze kumshangaa. Yaani msafiri mwenzao aliyetokea upande wanakotokea wao kuwa hajavisikia vituko vilivyotokea huko Yerusalemu.

Habari hizo zimevuma mji mzima na watu wote wanavizungumzia sana. “Inawezekanaje, wewe unayetoka sasa hivi huko mjini usisikie habari hii ya kusikitisha?”

Angekuwa mtu mwingine yeyote angeweza kuwasimamisha na kuwaambia: “Kaeni chini hapa niwaeleze kinaganaga cha mambo yalivyotokea.” Kumbe Yesu ameanza kwa kuwaamshia hamu ya kujieleza zaidi hadi wanamgeuzia kibao: “Hivi wewe peke yako ni mgeni asiyejua…”. Huwezi kujua ni jinsi gani Yesu alilipokea swali hilo la wafuasi. Swali hilo la wafuasi linaonesha waziwazi vionjo vilivyokuwa vimejaa ndani ya mioyo yao. Hadi hapo ilimtosha kabisa Yesu kujisikia kuaminiwa na watu hawa. Kleopa aliyekuwa katika hali mbaya ya kukata tamaa, na aliyejaa jazba, amefanikiwa kujimwaga mbele ya mgeni huyu.

Yesu anawaacha waendelee kujimwaga. Bila kujitambua wakaendelea kujieleza hadi kufikia kuzungumza mambo ya kiroho waliposema: “Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu yak ufa, wakamshulibisha… Tena wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona.” (Lk 24:19-20, 22-24).

Hapa unaona kama vile wamechanganyikiwa. Yaani, wanaonekana kwa upande mmoja kama vile wanasadiki lakini halafu kwa upande mwingine hawasadiki. Watu hawa wanateseka sana kisaikolojia lakini walikuwa bado na imani mioyoni mwao. Kwa hiyo Yesu anawaambia: “Enyi wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii!” (Lk.24:25).

Yaani, hawa walikuwa watu wa kutibiwa, siyo wa kuwalaani, watu wa kuwasahihisha na siyo kuwaachilia tu, watu wa kuwapoza siyo kuwagombeza! Baada ya kuwatulia kidogo, Yesu anaanza kuwapa dawa ya tiba. Anaanza kuwaelezea historia ya mambo yaliyokuwa kadiri ya Maandiko matakatifu hadi wanakaribia kijiji cha Emmaus.

Baadaa ya kumaliza kuwaeleza, Yesu angeweza kusema: “Sasa jamani baada ya kuwaeleza haya yote, tafadhali rudini Yerusalemu na mkawahabarishe wenzenu haya niliyowaambia ili msikose tena imani. Yesu hafanyi hivi badala yake anajifanya kama vile anapitiliza na kuendelea na safari zake. Hahitaji chochote, wala haulizi chochote, na wala hategemei chochote toka kwao. Ndiyo maana hawa wasafiri wawili wanaamua kumshawishi: “Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha.” (Lk 24:29). “Mgeni afike mwenyeji apone”. Je, sisi tumwambie nani “Kaa pamoja nasi”?

Tunaweza kumwambia mtu aliyetutendea jema fulani “kaa nasi”, au mgeni yule ambaye hatutii hasara, mtu asiyekuwa mzigo. Wageni namna hiyo wako wachache sana na pengine hawako kabisa. Kumbe Yesu aliye Mungu hahitaji chochote. Yesu aliyesukumwa na upendo mtupu hataki kumtuliza tu mtu. Hatukani mtu, hasemi maneno yasiyo na maana, huyu mgeni alitoa maneno ya kuhuisha. Aligusa hata mioyo yao, aliwatia moyo, hadi wanamkaribisha kwao.

“Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele.” (Lk 24: 28). Katika nafasi nyingine Yesu aliwapita wanafunzi wake: Mathalani kwenye mto Yordani, au mbele ya Yohane Mbatizaji kule Genesareti, au usiku ule wa dhoruba. Anapita pembeni ya Kanani bila kusimama. Anampita kipofu bila kumponya. Yesu anafanya hivi ili mmoja uweze kumtafuta, au uweze kumwita. Yesu anapenda kuitwa. Wakati mwingine anaweka hata mazingira ya kuja kwake na matendo yake ili aweze kuitwa na binadamu. Anavuvia, anadokeza, anashawishi, anahimiza lakini anasubiri. Wanafunzi wanamwomba atulie, abaki akae nao.

Wao wanahoja zao kinyume na ukweli ule wa ndani kabisa. Hoja wanayotoa ya kumshawishi abaki ni kwamba: “kumekuchwa, na mchana unakwisha.” Badala ya kumwambia kwamba tunapenda kuwa na wewe. Tumeshakupenda, licha ya kutukosoa na kutusahihisha, na hasa kutokana na hilo tunataka ubaki nasi. Yesu alilazimisha kwa wema. Alikuwa yeye wa kwanza kuwajongelea. Sasa wamekuwa wao kutaka kumshikilia asiondoke. Anaingia na katika tendo la kumega mkate, wanamtambua. Mioyo yao inafunguka: “Ni Yeye” wakasema. Lakini kabla hawajafanikia kuwasiliana naye, akawa ameshatoweka machoni pao.

Kumbe, ili aweze kutambulika, haoneshi vyeti vyake vya utambuilisho, na vyeti vya shule. Anajitambualisha kwa kumega mkate. Tendo ambalo wanafunzi wake wanamtambua mara moja. Yawezekana walimzoea akifanya hivyo kila walipokuwa wanakula pamoja. Aidha tendo hilo alilirudia karibuni tu kwenye karamu ya mwisho alipowaambia: “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.” (Lk. 22:19).

Hapo hapo wale wanafunzi wawili wakaanza safari ya kurudi Yerusalemu, wale ambao walipokuwa wanakuja Emaus walikuwa wamechoka, na kuchanganyikiwa. Sasa wanarudi kwa mbio wakiwa na kiherehere cha kwenda kuwasimulia wenzao kwamba Yesu amefufuka, anaishi, na kwamba wao wameonana naye. Waliochoka kutembea sasa wanakimbia.

Kumbe umoja aina hii na Kristu unaleta nguvu mpya na ari mpya. Tunaalikwa kutanguzana na Kristu katika maisha yetu.

P. Alcuin Nyirenda








All the contents on this site are copyrighted ©.