2014-05-03 07:55:19

Ujumbe wa Vatican kukutana na Kamati ya kudhibiti ukatili tarehe 5-6 Mei 2014


Kunako Mwaka 1984, Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa waliweka sahihi Mkataba dhidi ya ukatili, CAT. Vatican ikajiunga na kuridhia itifaki hii kunako mwaka 2002 na mwaka 2012, ikaanza kutoa taarifa ya utekelezaji wa mkataba huu. Akizungumzia kuhusu mkataba huu, Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, mkataba huu ni kati ya mikataba muhimu sana katika Jumuiya ya Kimataifa dhidi ya ukatili, dhuluma na nyanyaso kwa binadamu.

Ni mkataba ambao unazishirikisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa hiyari yao wenyewe na wala hakuna shuruti. Ili kuweza kuhakiki utekelezaji wa mkataba huu, Jumuiya ya Kimataifa imeunda kamati maalum ya wataalam wa kujitegemea, wanaoangalia utekelezaji wa mkataba huu kwa nchi zilizouridhia. Katika mkutano wake unaofanyika kila mwaka mjini Geneva, kamati hukutana na wajumbe wa nchi wanachama ili kujadiliana na kuona utekelezaji wake. Yote haya anasema Padre Lombardi hufanyika kwa njia ya majadiliano ya wazi yanayoweza kuvishirikisha vyama vya kiraia kwa njia ya kutoa maoni na mapendekezo yao

Kamati ya watu kumi ya Mkataba dhidi ya mateso inaendelea na kikao chake cha hamsini na mbili, kilichoanza hapo tarehe 28 Aprili na kitafungwa rasmi tarehe 23 Mei 2014. Mwaka huu kamati inachambua taarifa za utekelezaji wa mkataba huu kutoka katika nchi za: Uruguay, Thailand, Sierra Leone, Guinea, Montenegro, Cyprus, Lithuania pamoja na Vatican.

Mkutano wa kamati na wajumbe wa Vatican unafanyika Jumatatu tarehe 5 na tarehe 6 Mei, 2014. Wajumbe wa Vatican watawakilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa mkataba huu mjini Vatican na baadaye kutakuwa na maswali na ufafanuzi. Kamati itakuwa na taarifa kwa vyombo vya habari hapo tarehe 23 Mei 2014 na hapo itachapisha maoni na mapendekezo yake yatakayofanyiwa kazi baadaye na Vatican.

Padre Lombardi anasema kwamba, Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake limekuwa likitoa mkazo kuhusu umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, mambo ambayo yanafanyiwa rejea na Kamati dhidi ya ukatili na adhabu zinazokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Utekelezaji wa mkataba huu unahusu eneo la Vatican tu na wala si vinginevyo. Mapendekezo yaliyotolewa kwa Vatican kunako mwaka 2012 yalifanyiwa kazi kwa marekebisho ya sheria zilizoanza kutumika kunako mwaka 2013 kuhusu makosa ya jinai mjini Vatican.

Padre Federico Lombardi anasema, licha ya Vatican kuridhia na kufanya marekebisho katika sheria zake kadiri ya mapendekezo yaliyokuwa yametolewa, Vatican pia imeendelea kuridhia mikataba dhidi ya uhalifu wa kiuchumi na kifedha; ubaguzi wa rangi pamoja na haki za mtoto. Utekelezaji wa mapendekezo yaliyokuwa yametolewa na kamati unaonesha mafanikio makubwa.

Ni matumaini ya Vatican kwamba, wajumbe wa kamati watajielekeza zaidi katika masuala yanayogusa utekelezaji wa mkataba na wala si kufuata shinikizo linalotolewa na vyama vya kiraia kwa malengo binafsi ya kutaka kupata umaarufu kisiasa katika medani za kimataifa kama ilivyojitokeza wakati wa kusikiliza taarifa ya utekelezaji wa haki za mtoto mjini Vatican.

Kamati itekeleze wajibu wake kwa kuendesha majadiliano katika hali ya utulivu kwa kuzingatia malengo ya mkataba, vinginevyo anasema Padre Lombardi, kamati hii itakosa uhalali wake katika Jumuiya ya Kimataifa kwa kujikita katika masuala ya kisiasa badala ya kujielekeza zaidi katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Vatican itaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu dhidi ya ukatili na adhabu kali.







All the contents on this site are copyrighted ©.