Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari kuanza mkutano wake tarehe 5-10 Mei 2014 mjini
Roma
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu
pamoja na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari
ya Kipapa ni kati ya viongozi wakuu watakaotoa taarifa kwenye mkutano mkuu wa Mashirika
ya Kimissionari ya Kipapa katika mkutano wake mkuu wa mwaka unaoanza Jumatatu tarehe
5 hadi tarehe 10 Mei 2014. Mkutano huu unawashirikisha wakurugenzi wa Mashirika ya
Kipapa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Sehemu ya kwanza ya mkutano mkuu
ni kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 6 Mei 2014 kwa kujikita katika mikakati ya shughuli
za kichungaji. Hapa Makatibu wakuu wa Mashirika ya Kipapa wataangalia shughuli na
mikakati ya Uinjilishaji kati ya watu; mafundisho ya viongozi wakuu wa Kanisa na utekelezaji
wake katika Makanisa mahalia. Hapa Askofu mkuu Rugambwa na viongozi wenzake watatoa
ufafanuzi wa kina.
Sehemu ya pili itakayoanza hapo tarehe 7 hadi 10 Mei 2014
itashughulikia masuala ya kawaida ya Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa na wahusika
wakuu ni Makatibu wakuu wa Mashirika ya Kipapa kutoka mjini Vatican. Hawa wataangalia
taarifa na utekelezaji wa maazimio ya mwaka 2013, watapanga mwelekeo wa bajeti kwa
Mwaka 2014- 2015, msaada unaoombwa kutoka katika Makanisa mahalia; majadiliano na
hatimaye kupitisha miradi itakayokuwa imeridhiwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa Mashirika
ya Kimissionari ya Kipapa katika mkutano wao.
Ratiba elekezi inaonesha kwamba,
tarehe 9 Mei 2014 kutafanyika mikutano ya Mabara ili kupembua kwa kina na mapana maamuzi
yaliyofikiwa, kupitisha bajeti na miradi kadiri ya maeneo husika. Askofu mkuu Protase
Rugambwa anatarajiwa kutoa hotuba ya kufunga na Jumamosi, tarehe 10 Mei 2014 wajumbe
wanatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.