Jengeni na kudumisha mchakato wa urafiki na majadiliano ya kidini!
Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza Wakristo nchini Algeria kuwa ni kielelezo cha
Kanisa ambalo liko wazi kwa ajili ya kujenga na kudumisha mchakato wa urafiki na majadiliano
ya kidini, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu yuko karibu na
waamini wa Kanisa Katoliki nchini Algeria katika maisha na utume wao kwa kutambua
kwamba, wanaishi katika nchi ambayo ina idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam.
Hayo yamesemwa
na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini
katika Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya Miaka mia
moja tangu Kanisa la Mtakatifu Augustino lilipopewa hadhi ya kuwa Kanisa kuu, katika
Jimbo Katoliki la Costantina, nchini Algeria, tarehe 2 Mei 2014.
Katika mahubiri
yake, Kardinali Tauran anasema, Kanisa kuu lililojengwa nje ya Roma ni kielelezo cha
umoja na mshikamano na Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, lililoko mjini Vatican. Ni Kanisa
ambalo linapaswa kuwa na Mtakatifu msimamizi ambaye, waamini wanapaswa kufuata na
kuiga mfano wa utakatifu wa maisha yake.
Ndiyo maana, waamini wanachangamotishwa
na Kanisa kuiga mfano wa Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, aliyejitosa
kimasomaso kufundisha ukweli kwa kumwangalia mtu kutoka katika undani wa maisha yake.
Ni Mtakatifu anayeendelea kukazia umuhimu wa kujenga na kuimarisha: upendo ili kukuza
haki na amani; kugundua na kutambua uwepo wa Mungu kutoka katika undani wa maisha
ya kila mtu, katika uzuri wa mazingira na mawazo angavu yanayojikita katika urafiki
na mwingiliano wa watu!
Kanisa kuu la Mtakatifu Augustino lililokarabatiwa
katika kipindi cha miaka michache iliyopita bado linaonesha mawazo na mafundisho makuu
ya Mtakatifu Augustino kama mawe hai yanayopaswa kujenga na kuiimarisha Jumuiya ya
Wakatoliki, kwa kuendeleza uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake; majadiliano ya
kidini na waamini wa dini ya Kiislam pamoja na kushirikiana na wote katika kutafuta
mafao na ustawi wa wananchi wote wa Algeria.
Kanisa kuu la Mtakatifu Augustino,
liwe ni kielelezo chenye mvuto na mashiko kwa watu wenye kiu ya kutaka kukutana na
kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao, ili waweze kupata
mahali nyumba ambamo wanaweza kusali katika mchakato wa kutafuta ukweli, upendo na
uhuru, tema ambazo ni msingi katika mafundisho ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu
wa Kanisa.
Kardinali Tauran anasema, Mtakatifu Augustino alipambana kwa ujasiri
mkubwa na changamoto zilizojitokeza wakati wa uhai wake, kama ilivyo kwa wakati huu
ambapo kuna mabadiliko makubwa ya kitamaduni na kisiasa, changamoto kwa waamini na
watu wote wenye mapenzi mema kuyaangalia yote haya kwa jicho la moyo, kwa kusikiliza
kilio cha binadamu katika ulimwengu mamboleo!
Hawa ni watu wasiokuwa na fursa
za ajira; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha;
ni watu waliosahaulika, wafungwa na wote wanaoteseka! watu hawa waguswe na utakatifu
pamoja na hekima ya Mtakatifu Augustino.